Habari

Korti sasa yataka Uhuru na Raila kuandikisha taarifa

July 2nd, 2020 2 min read

RICHARD MUNGUTI na BENSON MATHEKA

MAHAKAMA Alhamisi imeagiza afisa anayechunguza kesi dhidi ya watu wawili walioshtakiwa kwa dai la kusambaza kanda ya video inayoonyesha Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga wakitembea jijini usiku, aandikishe taarifa za viongozi hao.

Washukiwa hao ambao ni wafanyakazi wa hoteli ya New Stanley jijini Nairobi wameshtakiwa kwa kusambaza video hiyo iliyoonyesha viongozi hao wawili wakiwa katika barabara za jiji.

Mahakama ilimpatia afisa huyo muda wa siku saba kuandikisha taarifa kutoka kwa Rais Kenyatta na Bw Odinga.

Hata hivyo, huenda hatua hiyo ikachelewesha kesi ikibainika kuwa si rahisi kumfikia kiongozi wa nchi huku Bw Odinga akiwa anaugua.

Hakimu mkazi Zainab Abdalla alimwamuru afisa huyo arekodi taarifa za ushahidi kutoka kwa Rais Kenyatta na Bw Odinga ndipo zikabidhiwe washtakiwa wajiandae kujitetea.

Bi Abdalla aliamuru afisa huyo awasilishe taarifa kortini Julai 9, 2020.

Mahakama ilifahamishwa na mawakili Danstan Omari na Apollo Mboya kwamba Patrick Rading Ambogo na Janet Magoma Ayonga hawajui jinsi ya kuandaa tetesi zao kwa vile hawajapokea taarifa za ushahidi za walalamishi wawili Rais Kenyatta na Bw Odinga.

“Washtakiwa hawa wawili hawana amani kamwe kwa vile hawajui jinsi ushahidi wa Rais Kenyatta na Bw Odinga ambao ndio walalamishi ulivyo,” alisema Bw Omari.

Mawakili hao walisema tangu Ambogo na Magoma wafikishwe kortini wiki mbili zilizopita “hawajapewa nakala za mashahidi ndio wajue madai dhidi yao.”

Bw Omari alisema waliomba afisa anayechunguza kesi dhidi ya wawili hao awape kanda halisi iliyonakili Rais Kenyatta na Bw Odinga wakitembea katika barabara ya Kenyatta Avenue usiku wa Juni 2, 2020.

Mawakili hao walieleza mahakama kuwa washtakiwa wanataka kuanza kuandaa ushahidi wao, lakini hawawezi kwa vile hawajakabidhiwa nakala za mashahidi.

Wawili hao wanakabiliwa na shtaka la kusambaza video iliyonakiliwa na kamera za CCTV za hoteli ya New Stanley ikionyesha Rais Kenyatta na Bw Odinga wakitembea katika barabara ya Kenyatta Avenue usiku.

Shtaka linasema washtakiwa walisambaza video hiyo inayoonyesha msafara wa magari ya Rais Kenyatta bila idhini.

Akitoa uamuzi, Bi Abdalla aliamuru afisa anayechunguza kesi hiyo arekodi ushahidi kutoka kwa walalamishi hao wawili bila kusita.

Hakimu aliamuru kesi hiyo itajwe tena Julai 9, 2020, ndipo nakala za mashahidi ziwasilishwe kortini na kukabidhiwa washtakiwa.

Kurekodi taarifa kutoka kwa Rais, kutahitaji mipango maalumu na inaweza kufanywa na Inspekta Mkuu wa polisi na hii itategemea iwapo Rais atakubali.

Na iwapo wataandikisha taarifa zao, viongozi hao watalazimika kufika kortini kuhojiwa na mawakili wa washtakiwa kesi itakapokuwa ikisikilizwa, jambo ambalo kwa Rais halitawezekana.

Sheria ya kesi za uhalifu inasema washtakiwa wanapaswa kukabidhiwa nakala za taarifa za mashahidi na ushahidi wote kutoka upande wa mashtaka kabla ya kesi kuanza ili wajiandae kwa kesi.

Washtakiwa walikanusha shtaka dhidi yao na waliachiliwa kwa dhamana ya Sh50,000 kila mmoja.