Habari Mseto

Korti yaagiza Boinnet afurushe Mnigeria kipenzi cha wanawake jijini

April 11th, 2018 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

HAKIMU mkuu katika mahakama ya Nairobi Bw Francis Andayi, Jumatano alimwamuru Mkuu wa Polisi (IG) Joseph Boinnet pamoja Idara ya Uhamiaji wamfurushe kutoka humu nchini raia wa Nigeria anayedaiwa kuwa mwizi wa magari na mwenye mazoea ya kuishi na wanawake tofauti tofauti.

“Mshtakiwa huyu Okeke Patrick Godwin Chukwudi (pichani) asafirishwe mara moja atoke mbele yangu hadi nchini Nigeria,” Bw Andayi alimwagiza IG.

Hakimu alisema Bw Chukwudi hana kitambulisho chochote hawezi kukubaliwa kuishi humu nchini.

Raia huyo wa kigeni aliyekabiliwa na shtaka la kupatikana bila cheti cha kumruhusu kuishi humu nchini alijitetea akisema kwamba: “ Nimeishi hapa nchini tangu mwaka wa 2010 na hata nimeomuoa mwanamke raia wa Kenya.”

Alimweleza hakimu kwamba mwanamke aliyekuwa akiishi naye alimwibia gari na pasipoti yake na “sasa hana hati yoyote ya kunitambulisha.”

Lakini kiongozi wa mashtaka Bw Solomon Naulikha alimweleza hakimu kwamba mshtakiwa alitiwa nguvuni na polisi akiendesha gari iliyo na nambari za usajili za humu nchini nambari KCE 128H.

“Naomba hii korti inionee huruma kwa vile mwanamke niliyekuwa nimemuoa raia wa Kenya Valentine Arigi aliniibia gari na pasipoti. Sasa sina hati yoyote ya kunitambua,” mshtakiwa alijitetea.

Lakini Bw Naulikha alimweleza hakimu kwamba mshtakiwa hana makao maalum kwa vile “yuko na tabia ya kuhama kutoka kwa mwanamke mmoja hadi kwa mwingine.”

Bw Naulikha alipinga mshtakiwa akiachiliwa kwa dhamana akisema “atoroka na hatafika kortini siku ya kusikizwa kwa kesi kwa vile hana makao maalum.”

Mahakama iliamuru IG na Idara ya Uhamiaji amsafirishe mshtakiwa hadi nchini Nigeria na kumkabidhi kwa wizara ya kigeni apelekwe alikozaliwa katika jimbo la Ibo.

Bw Chukwudi alidaiwa kwamba alipatikana humu nchini bila kibali cha kumruhusu kuishi mnamo Aprili 9, 2018.