Habari Mseto

Korti yaagiza mshukiwa wa wizi wa magari akimbizwe hospitalini

May 26th, 2018 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA imeamuru mshukiwa wa wizi wa magari Yassin Muli Muthama (pichani kulia) apelekwe hospitalini mara moja kutoka gerezani.

Muli aliyekuwa amepata ajali alikuwa amevimba uso kupindukia.

Macho yote yalikuwa yameshikana kwa kuvimba.

“Mshtakiwa alikuwa amevimba hivi siku ile alikuwa hapa kortini Jumatatu? Hakimu mkazi Bi Miriam Mugure alimwuliza wakili David Ayuo anayewatetea.

“Hapana. Alikuwa hajavimba hivi lakini niliomba korti imwachilie kwa dhamana aende hospitali. Sasa ameumia zaidi akiwa gerezani,” alijibu Bw Ayuo.

Mahakama ilimwonea mshtakiwa huyo huruma na kumwachilia kwa dhamana ya Sh100,000 pesa tasillimu mbali na kuamuru apelekwe hospitali mara moja.

Kesi itatajwa Mei 29, 2018.

Yasin  ameshtakiwa pamoja na Bw Mbithi Munyao.

Walidaiwa mnamo Mei 21 katika mtaa wa Magiwa kaunti ya Nairobi waliiba magari mawili  miundo ya Probox yenye thamani ya Sh700,000 mali ya Bi Christine Gataka.

Pia walikana waliiba gari lingine muundo wa Toyota Allion lenye thamani ya Sh1.2milioni lake Bw Humphrey Otieno Olima.

Upande wa mashtaka ulipinga Yasin akiachiliwa kwa dhamana kwa madai aliiba magari haya akiwa nje kwa dhamana.

Yasin anadaiwa anakabiliwa na kesi nyingine mbele ya hakimu mkuu Francis Andayi