HabariSiasa

Korti yaagiza Nyong’o na dadake wafungwe jela

July 25th, 2019 2 min read

NA RUSHDIE OUDIA

GAVANA wa Kisumu Prof Anyang’ Nyong’o, amejipata matatani tena baada ya Mahakama Kuu ya Kisumu kutoa amri akamatwe pamoja na dadake kwa kukiuka agizo la korti kwenye kesi ya urithi wa mali ya familia.

Jaji Tripsisa Cherere Alhamisi alitoa amri kwa Kamanda wa Polisi Kaunti ya Kisumu Benson Maweu kumkamata Prof Nyong’o na dadake Dkt Risper Nyagoy na pia ikawapa hukumu ya mwezi mmoja gerezani baada ya kupatikana na hatia ya kukiuka amri iliyotolewa awali.

Mnamo Oktoba 11, 2018, wawili hao waliagizwa kuleta vitabu vya uhasibu wa fedha zinazotokana na mali ya babake gavana huyo, marehemu Hesbone Shimei Nyong’o lakini wakapuuza amri hiyo.

Prof Nyong’o na Dkt Nyagoy pia walipatikana na hatia ya kukaidi amri ya korti iliyowaamrisha wajumuishe wapwa wao kwenye orodha ya wanafamilia ambao wanafaa kufaidi mali ya marehemu baba yao.

Mali ambayo imezua mzozo kwenye familia ya gavana huyo inakadiriwa kuwa zaidi ya Sh200 milioni na inajumuisha ekari 100 za ardhi eneo la Miwani, nyumba za kukodisha karibu na barabara za Jogoo jijini Nairobi na vipande vya ardhi katika mitaa ya Manyatta, Tamu, Milimani na nyumbani kwao Rata, Seme, Kaunti ya Kisumu.

“Uamuzi wa korti ni wa haki. Jaji amedhihirisha kwamba anafuata sheria bila kuzingatia hadhi ya mtu katika jamii,” akasema wakili wa wapwa wa gavana huyo, Bw Rogers Mugumya.

Mnamo Mei 30, baada ya kukataa kufuata amri ya awali, korti iliwaamrisha Dkt Nyagoy na Prof Nyong’o walipe faini ya Sh400,000 kila moja katika muda wa siku 30 kwenye kesi hiyo iliyowasilishwa dhidi yao na wapwa wao Kenneth Okuthe na Omondi Nyong’o.

Hata hivyo, wawili hao walikosa kulipa fedha hizo kwa muda huo ndipo Jaji akawahukumu mwezi moja gerezani kwenye kikao cha jana. Kando na hayo, korti pia iliwaamrisha walipe Sh50,000 kwa kila mwezi ambao watakosa kuwasilisha vitabu vya hesabu kuhusu fedha za mali ya baba yao.

Katika kikao cha jana wakili wa Prof Nyong’o aliomba mteja wake apewe muda zaidi kutimiza amri ya korti akisema bado wanangoja ombi la kupinga mashtaka dhidi yao waliyowasilisha katika mahakama ya rufaa lisikizwe na kuamuliwa.