Habari MsetoSiasa

Korti yaambiwa Itumbi aliandika barua feki kuhusu mauaji ya Ruto

July 22nd, 2019 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

AFISA wa mawasiliano katika afisi ya naibu wa rais Dennis Itumbi hatimaye alishtakiwa Jumatatu baada ya mahojiano yaliyochukua zaidi ya mwezi mmoja kuhusu madai ya njama za kuuawa kwa naibu wa Rais William Ruto.

Bw Itumbi alifunguliwa mashtaka matatu, huku korti ikiambiwa shataka kuu ni kutengeneza barua feki iliyozua mtafaruku miongoni mwa idara mbalimbali za Serikali.

Bw Itumbi alikanusha mashtaka matatu yaliyowasilishwa na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji kuhusu barua hiyo iliyoyumbisha baraza la mawaziri na kutishia umoja serikalini.

Itumbi alifikishwa mbele ya hakimu mwandamizi katika mahakama ya Milimani Nairobi Bw Kennedy Cheruiyot.

Aliyakana mashtaka yote dhidi yake na kiongozi wa mashtaka Bi Jacinta Nyamosi akaomba mahakama imwamuru asizugumzie suala la barua hiyo katika mitandao yao kijamii.

“Mashtaka aliyoshtakiwa Itumbi ni makali na adhabu yake pia. Naomba mahakama imwachilie kwa masharti makali,” Bi Nyamosi aliirai mahakama.

Kuhusu kuzimwa kujadilia suala la barua hiyo hakimu alishangaa ni Bw Itumbi peke yake anayepasa kuzimwa au ni kila mmoja nchini.

“Je, ni Bw Itumbi peke yake anayepasa kuzimwa kujadilia suala hili ama kila mmoja ambaye amekuwa akilizugumzia.? Bw Cheruiyot alimwuliza Bi Nyamosi.

“Ni kila mmoja ambaye amelikuwa akilizugumzia. Kwa upande wa Itumbi, ambaye ni muhusika mkuu anapasa kuzimwa kabisa kuijadilia katika mitandao ya kijamii,” alijibu Bi Nyamosi.

Wakili Katwa Kigen aliyemwakilisha Itumbi pamoja na Moses Cheleng’a alipinga Bw Itumbi akizimwa peke yake kuzugumzia suala hili ama kuichapisha katika mitandao ya kijamii.

Bw Kigen alieleza mahakama kuwa , mshtakiwa alikuwa ameachiliwa kwa dhamana ya Sh100,000 na hakimu mkazi Bi Zainabu Abdul wiki mbili zilizopita.

“Mshtakiwa aliachiliwa kwa dhamana ya Sh100,000 na kuagizwa awasilishe pasipoti yake kortini mbali na kuzimwa kujadili suala hili katika mitandao ya kijamii,” alisema Bw Kigen.

Wakili aliongeza kila mmoja anapasa kuzimwa kujadilia suala hili katika hafla za umma na pia katika mitandao ya kijamii.

Akitoa uamuzi, Bw Cheruiyot aliamuru masharti ambayo Bw Itumbi alipewa na Bi Abdul yatasalia tu.

Alimtaka Bw Itumbi asijadilie suala barua hiyo katika mitandao ya kijamii.

Pia alizima kila mwananchi mwingine dhidi ya kulizugumzia hilo suala katika hafla mbali mbali.

Aliorodhesha kesi kusikizwa Septemba 2, 2019.

Itumbi alikabiliwa na shtaka la kutengeneza barua feki mnamo Juni 20,2019 akidai ilikuewa imeandikwa na Waziri wa Serikali mnamo Mei 30, 2019.

Shtaka la pili lilisema alichapisha barua hiyo katika mitandao ya kijamii na kuzua hisia kali miongoni mwa umma.

Shtaka la mwisho lilisema alikarabati simu yake ya Samsung kinyume cha sheria.