Habari Mseto

'Mshukiwa amekuwa akiwasiliana na Al-Shabaab'

July 22nd, 2019 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MSHUKIWA wa ugaidi aliyekamatwa katika Uwanja wa Ndge wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) Ijumaa wiki iliyopita alifikishwa kortini Jumatatu.

Ishmael Mano Otieno alikana mashtaka 11 mbele ya hakimu mwandamizi Kennedy Cheruiyot.

Mano mwenye umri wa miaka 23 aliamriwa azuiliwe katika gereza la viwandani hadi Ijumaa atakaporudi kortini kujibu ombi la kiongozi wa mashtaka anyimwe dhamana.

Kiongozi wa mashtaka Angela Odhiambo aliomba mahakama imnyime dhamana mshtakiwa kwa vile makosa yanayomkabili ni mabaya na adhabu yake ni kifungo cha maisha endapo atapatikana na hatia.

Mano aliomba muda asome mawasilisho ya Bi Odhiambo kuhusu kesi inayomkabili ya kupatikana katika uwanja wa JKIA akiwa mwanachama wa kundi la magaidi la Al Shabaab.

Mahakama ilifahamishwa mshtakiwa alikutwa na simu iliyokuwa na picha na taarifa zinazothibitisha amekuwa akiwasiliana na magaidi wa Al Shabaab.