Korti yaamua wajane wana haki kurithi mali wakiolewa tena

Korti yaamua wajane wana haki kurithi mali wakiolewa tena

NA DAVID MUCHUI

WAJANE wana haki ya kurithi mali ya marehemu waume wao hata wakiolewa tena, Mahakama Kuu imeamua.

Mahakama Kuu ya Meru imebatilisha sehemu kadha za Sheria ya Urithi wa Mali ya Marehemu zilizowanyima wajane haki ya kurithi mali ya waume zao baada ya kuolewa tena.

Jaji Edward Murithi, katika uamuzi alioutoa Alhamisi, alielekeza kwamba sehemu ya 35 (1) (b) na sehemu ya 36 (1) (b) ya sheria zinakiuka Katiba.

Alitoa uamuzi huo kufuatia kesi iliyowasilishwa kortini na shirika la Ripple International mwaka 2021.

Shirika hilo lisilo la kiserikali, lenye makao yake makuu mjini Meru, hulinda na kutetea haki za wajane na watoto katika kaunti hiyo.

Kulingana kesi hiyo, sehemu za 35 na 36 za sheria hiyo ya urithi ni batili kwa sababu zinawanyima wajane haki ya kurithi mali za wanaume zao waliofariki, ikiwa wataamua kuolewa kwa mara nyingine.

Shirikisho la Mawakili Wanawake (Fida) na shirika la Inua Mama Mjane, zilishirikishwa katika kesi hiyo kama wahusika.

Katika kesi hiyo, Ripple International ilihoji uhalali wa sehemu za 32, 35 (1) (b), 36 (1) (b) na 39 (1) (b) za sheria hiyo ya urithi wa mali ya mwendazake.

Lakini Jaji Muriithi aliamua kuwa mlalamishi alipaswa kuwasilisha ushahidi wenye uzito utakaowezesha kubatilishwa kwa sehemu za 32 na 33 za sheria hiyo.

Jaji huyo hakutoa uamuzi wake kuhusu sehemu za 39 (1) (b) ambayo aliahidi kushughulikia baada ya wakili wa Ripples International Samson Macharia kutaja dosari iliyopo.

“Mwanasheria Mkuu atapata nakala ya uamuzi huu na anaweza kuchukua hatua ambayo anadhani ni sawa,” Jaji Murithi akaamuru.

Sehemu ya 32 ya sheria hiyo inahusu mali iliyoachwa nje ya sheria inayofaa kufuatwa endapo mtu atakufa bila kuacha wosia.

Mali iliyoachwa nje kulingana na sehemu hiyo, ni ardhi inayotumika kuendeshea kilimo au ufugaji mifugo katika kaunti za Pokot Magharibi, Turkana, Marsabit, Mandera, Wajir, Garissa, Tana River, Narok, Samburu, Isiolo, Lamu na Kajiado.

Sheria hiyo inasema kuwa sheria ya jamii ya mwendazake itatumika katika maeneo yaliyoorodheshwa, ikiwa mtu aliaga dunia bila kuacha wosia.

Ripples International ililalamika kuwa Sehemu ya 32 ya sheria hiyo ya urithi inakiuka vipengele vya katiba vinavyohimiza usawa na kulindwa kwa haki na uhuru wa wajane.

“Serikali haifai kubagua mtu yeyote kwa misingi ya rangi, jinsia, uja uzito, ndoa, afya, hadhi, kabila, umri, ulemavu, dini, hisia, imani, mavazi, lugha au mahala pa kuzaliwa,” mlalamishi alisema.

Shirika hilo lilisema kuwa kipengele cha 45, ibara za (2) na (3) za Katiba zinalinda haki ya mtu kuoa au kuolewa huku zikilinda usawa kati ya washirika katika ndoa.

“Hii ina maana kuwa sheria yoyote inayohujumu haki ya mshirika mmoja katika ndoa au usawa katika ndoa kwa kubagua mmoja wao, inakwenda kinyume cha Katiba,” shirika hilo likasema.

  • Tags

You can share this post!

Hakikisho wafanyakazi 6,021 NMS wataajiriwa na serikali ya...

Masharti makali ya kutoshiriki ngono waliopona Ebola

T L