Habari Mseto

Korti yaamuru mkewe Linturi arudi kwa makazi ya Runda

January 10th, 2019 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA kuu Jumatano ilimwamuru mkewe Seneta wa Meru Mithika Linturi, Bi Maryanne Chebet Kitany arudi mara moja katika makazi yao ya kifahari mtaani Runda kaunti ya Nairobi.

Jaji John Onyiego alimwagiza afisa mkuu katika kituo wa Polisi cha Runda (OCS) ahakikishe Kitany amerudi na kuishi katika makazi yao na mumewe kwa amani.

Na wakati huo huo mahakama iliamuru walinzi wanaolinda makazi hayo waondolewe mara na “ Linturi na mkewe waajiri walinzi wapya.”

OCS wa Runda aliamriwa awaondoe maafisa wa polisi na mabawabu kwenye makazi hayo hadi “ walinzi wengine waajiriwe.”

“ Namwamuru OCS Runda ahakikishe maagizo ya hii mahakama yametekelezwa na Maryanne amerudi katika makazi yake kirasmi,” Jaji Onyiego.

Jaji Onyiego alikashfu kitendo cha Bw Linturi kumtimua kwa nyumba mkewe kwa njia ya ukatili na kuamuru “ OCS ahakikishe mlalamishi (Bi Kitany) amerudi katika makazi yao pasi kusumbuliwa hadi kesi ya uhalali wa ndoa yao iamuliwe na mahakama ya Meru.”

Bi Kitany alikuwa amemshtaki mumewe Bw Linturi akiomba akubaliwe kurudi kuishi katika makazi yao mtaani Runda na kuruhusiwa kutumia magari yao na hata kutoa pesa katika akaunti zao.

Wakili Danstan Omari aliyewasilisha kesi hiyo katika mahakama kuu alisema kuwa Bi Kitany ni mke halisi wa Seneta Linturi , aliyeolewa kwa mujibu wa sheria za kitamaduni cha Jamii ya Ameru na wameishi kama mke na mume hadi pale ambapo tofauti baina yao zilipoanza kuchipuka.

Mahakama ilielezwa na Bw Omari kwamba mlalamishi (mkewe linturi) yuko na kila haki ya kuishi katika nyumba hiyo kwa vile alisaidia kuijenga na “ hata ramani ya jumba hilo la kifahari limechorwa na kuandikwa jina la Maryanne Chebet Kintany.”

Mahakama iliombwa ifikie uamuzi kwamba wawili hao ni wamiliki wa pamoja wa jumba hilo lao la kifahari ambapo wamekuwa wakiishi raha mstarehe.

“Naomba hii mahakama itilie maanani kwamba watoto wa Maryanne hawajajiunga na wanafunzi wengine tangu shule zilipofunguliwa kwa vile vitabu , sare za shule na mifuko imefungiwa katika nyumba hiyo na Seneta Linturi,” alisema Bw Omari.

Lakini Bw Linturi , kupitia kwa wakili Muthomi Thiankolu, alipinga mlalamishi akirudi katika makazi hayo akidai “ Maryanne alikuwa mgeni wa seneta huyo na kwamba hawezi kukubaliwa kuendelea kuishi katika makazi hayo.”

Akitoa uamuzi wake , Jaji Onyiego alisema, ushahidi uliowasilishwa na naibu wa Msajili wa mahakama kuu aliyetembelea makazi hayo alitambua kuwa “ Maryanne na watoto wake walikuwa wakiishi katika makazi hayo ya kifahari.”

“Ni wazi Maryanne na watoto wake wamekuwa wakiishi katika makazi hayo ya Runda,” alisema Jaji Onyiego na kuongeza, “Baada ya Linturi kumtaliki mkewe wa kwanza alifunga pingu za maisha na Maryanne na “ wamekuwa wakiishi kama mke na mume.”

Korti ilisema masuala mengine kuhusu ndoa yao yataamuliwa kesi inayoendelea katika mahakama kuu ya Meru itakapoamuliwa.