Michezo

Korti yaamuru Neymar ailipe Barca Sh854 milioni

June 20th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

FOWADI Neymar Jr wa Paris Saint-Germain (PSG) ameamrishwa na korti kuwalipa waajiri wake wa zamani, Barcelona, kima cha Sh854 milioni.

Hii ni baada ya nyota huyo kupoteza kesi ambapo aliwahi kudai kwamba Barcelona walistahili kumlipa bonasi za kima cha Sh4.8 bilioni kabla ya kuagana na miamba hao wa soka ya Uhispania mnamo Agosti 2017.

Jaji aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo alisema kwamba Neymar, 28, alishindwa kushawishi waendeshaji wa mashtaka waliompata na hatia ya kudai fidia isiyostahili kutoka kwa Barcelona japo wapo huru kukata rufaa dhidi ya maamuzi dhidi yake.

Kwa upande wao, Barcelona walifurahia hukumu hiyo na wakasema wataendelea “kupigania haki za kikosi chao kadri ya uwezo wao siku zote”.

Neymar aliwasilisha malalamishi ya “kukandamizwa na Barcelona” kwa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) mnamo 2017 baada ya kudai kwamba miamba hao walistahili kumlipa kima cha Sh4.8 bilioni na asilimia kubwa ya Sh28 bilioni zilizotolewa na PSG walipokuwa wakimsajili.

Zaidi ya kutomlipa Neymar, Barcelona pia walianzisha mchakato wa kisheria dhidi ya sogora huyo na wanamtaka sasa arejeshe kima cha Sh1.2 bilioni ambazo Neymar alipokezwa baada ya kutia saini mkataba mpya uwanjani Nou Camp mnamo 2016.

Licha ya kupokea malalamishi ya Neymar, FIFA walisisitiza kwamba hawana uwezo wa kuchukua hatua yoyote ila kuacha kesi hiyo isikilizwe na kuamuliwa na mahakama.