Korti yaamuru raia wa Tanzania anayeishi uingereza akamatwe arudishwe Kenya kushtakiwa kwa ufisadi wa Sh706Milioni

Korti yaamuru raia wa Tanzania anayeishi uingereza akamatwe arudishwe Kenya kushtakiwa kwa ufisadi wa Sh706Milioni

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA Jumatano iliwaagiza maafisa wa polisi nchini wamkamate mfanyabiashara raia wa Tanzania anayeishi nchini Uingereza anayesakwa kwa kula njama za kuifilisi benki moja nchini Kenya Sh706milioni.

Hakimu mwandamizi mahakama ya Milimani Bw David Ndungi aliagiza maafisa wa polisi washirikiane na polisi wa kimataifa kumtia nguvuni Bw Gaurav Jayeshkumar Kotecha kutoka Uingereza.

Bw Ndungi alikuwa amemwamuru Bw Kotecha kupitia kwa wakili wake Nelvile Amolo afike kortini Septemba 29, 2021 kujibu shtaka la kula njama za kuifilisi benki ya Prime Bank Limited Sh706,989,273.

Benki hii ilikuwa imeipa kampuni ya Midland Hauliers Limited mkopo wa zaidi ya Sh700milioni.Midland Hauliers Ltd ilikuwa imetumia malori yake manne KBJ 990X, KBK 090P,KBJ 990S na KBV 621V kama dhamana  katika benki ya Prime kukopa pesa.

Kiongozi wa mashtaka Bw Abel Omariba aliomba mahakama itoe kibali cha kumkamata Bw Kotecha kwa vile alikataa kufika kortini kujibu shtaka kwa sababu ya utundu tu.

Hakimu mwandamizi David Ndungi…PICHA/RICHARD MUNGUTI

Bw Omariba alieleza mahakama kuwa mshtakiwa huyo alikuwa amepewa samanzi afike kortini lakini alikataa kufika .Mahakama ilisema kuwa pia mshtakiwa hakuwasilisha kortini cheti kuonyesha alikuwa anaugua ugonjwa wa Covid-19.

Mahakama ilisema korti iliamini ushahidi wa wakili Nelvile Amolo kwamba angelimfikisha kortini jana.Mahakama iliagiza kesi hiyo itajwe Novemba 5, 2021.

Bw Kotecha aliagizwa afike kortini siku  hiyo kujibu mashtaka ya kula njama za kuilaghai Prime Bank Sh706miliioni kwa kuuza malori manne yaliyokuwa yametumika kudhamini mkopo huo.

Bw Kotecha pamoja na  Jayeshkumar Prabhudas Kotecha wameshtakiwa kuuzia malori hayo kampuni ya Super Hakika Ltd kutoka kwa Midland iliyokuwa imewekwa chini ya usimamizi wa mrasimu.

  • Tags

You can share this post!

Mawakili wa SNOLEGAL waambia Omanyala baibai siku tatu...

KINYUA BIN KINGORI: Vyama vya kisiasa vinavyoendesha...