Uncategorized

Korti yaamuru wajakazi wa Wanjigi watibiwe maradhi ya kuharisha ‘waliyoambukizwa rumande’

Na RICHARD MUNGUTI August 14th, 2024 1 min read

POLISI wameagizwa na mahakama wawapeleke Hospitali Kuu ya Kenyatta (KNH) vibarua wanne waliokamatwa nje ya makazi ya mwanasiasa Jimi Wanjigi kutibiwa ugonjwa wa kuhara walioambukizwa wakiwa rumande.

Wanne hao wanachunguzwa kwa madai ya kupatikana na grunedi nne.

Hakimu mkuu Bernard Ochoi aliamuru Kennedy Ochieng Asewe, Joseph Augo Otimo, Dancan Otieno na Calvin Odhiambo Odongo wapelekwe KNH baada ya kulalamika kortini “wanahara na kuumwa na tumbo.”

“Chakula tulichopewa tukiwa rumande katika kituo cha polisi cha Central kimetudhuru. Tunahara, kuumwa na kusokotwa na tumbo. Naomba hii mahakama iamuru tupelekwe KNH kutibiwa,” Otieno alimweleza Bw Ochoi.

Mawakili Willis Otieno, Dkt Owiso Owiso, Ian Mutiso na John Andati walieleza mahakama kwamba madai ya washukiwa hao hayapasi kupuuzwa kwa vile “matibabu ni haki ya kila Mkenya.”

Akiomba polisi waagizwe wawapeleke vibarua hao KNH, Bw Otieno alisema suala la afya ni jambo la dharura.

Wakili huyo alisema chakula walichopewa vibarua hao kimewadhuru na “wanahitaji matibabu ya dharura.”

Upande wa mashtaka ukiongozwa Mabw James Gachoka na Herbert Sonye haukupinga ombi hilo wakisema “kila mmoja anatakiwa kuwa buheri wa afya.”

“Wapelekwe Hospitali,” Bw Sonye alimweleza hakimu.

Bw Ochoi alimwamuru afisa anayechunguza kesi dhidi ya Asewe, Otimo, Otieno na Odongo awapeleke KNH kupokea matibabu.

Hakimu alitoa agizo hilo baada ya kuruhusu polisi wawazuilie washukiwa hao kuwahoji kuhusu grunedi hizo.

Wanne hao walikamatwa Agosti 8, 2024 baada ya polisi kudai walipata grunedi ndani ya gari walimokuwa.

Ilikuwa imeegeshwa nje ya makazi ya Wanjigi.

Kesi hiyo itatajwa Agosti 19, 2024.