Korti yacharaza Uhuru kiboko mara nyingine ikisema alipuuza Katiba

Korti yacharaza Uhuru kiboko mara nyingine ikisema alipuuza Katiba

Na RICHARD MUNGUTI

RAIS Uhuru Kenyatta amepata pigo jingine katika maamuzi yake baada ya Mahakama Kuu jana kufutilia mbali uteuzi wa wakuu 129 wa mashirika ya serikali na bodi, ikisema ulifanywa kinyume cha sheria.

Majaji Jessie Lesiit, Chacha Mwita na Lucy Njuguna walisema teuzi hizo zilizofanywa na Rais Uhuru Kenyatta na baadhi ya mawaziri mnamo 2018, hazikufanywa kuambatana na Katiba kwa kuwa maoni ya umma hayakushirikishwa.

Waliongeza kuwa hakukuwa na ushindani katika teuzi hizo kwa vile hakuna watu walioomba kazi hizo.

Miongoni mwa wakuu wa mashirika ambao uteuzi wao umeharamishwa ni pamoja na aliyekuwa Mkuu wa Majeshi Julius Karangi.

Wengine ni wale walioshindwa katika uchaguzi mkuu wa 2017 wakiongozwa na Bw Benjamin Cheboi aliyewania Ugavana Baringo na Bw Godana Doyo (Isiolo).

Wengine ni aliyewania Ugavana Mombasa Suleiman Shabhal, mjane wa George Saitoti Margaret Wanjiru Saitoti, bintiye rais mstaafu Mwai Kibaki Bi Judith Wanjiku na aliyekuwa mwenyekiti wa chama cha kitaifa cha kutetea walimu (Knut) Mudzo Nzili na aliyekuwa afisa mkuu wa afya kaunti ya Nairobi Dkt Washington Makodingo.

Pia aliyekuwa Mbunge wa Ndhiwa Augustino Neto aliathiriwa na uamuzi huo.

Uamuzi huo wa Mahakama Kuu umefanyika wiki mbili tu baada ya mahakama hiyo hiyo kuzima mchakato wa BBI ikisema ni haramu.

Kezi zingine ambazo mahakama imeamua kuwa Rais Kenyatta amekiuka Katiba ni pamoja na hatua yake kukataa kuwaapisha majaji 4i, kumzuia Miguna Miguna kurudi nchini kutoka Canada na ubomoaji wa makao katika mtaa wa Kariobangu mwaka jana.

Mahakama pia imebatilisha hatua za rais kukabidhi kiwanda cha nyama cha Kenya Meat Commission kwa Idara ya Jeshi (KDF) na kukabidhi usimamizi wa jiji la Nairobi kwa NMS.

You can share this post!

Mwanamke atoroka mumewe na kuolewa na ‘roho mtakatifu’

Wapingao BBI wataka rufaa isikizwe na majaji 11