Habari Mseto

Korti yadinda kumlazimisha Betty Tett kutambua wazazi wa mwana wa kambo

April 19th, 2018 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA Kuu Jumatano ilikataa kuwashurutisha aliyekuwa Waziri msaidizi Bi Betty  Tett na mumewe William Mulready Tett kuwatambua wazazi waliomzaa mwanao wa kambo David William Tett.

David aliyehukumiwa kunyongwa kwa kumnyang’anya kimabavu Mukready katika kisa ambapo majambazi wawili waliuawa, alikuwa amewasilisha kesi katika mahakama kuu akiomba wazazi hao wake wa kambo walazimishwe kumtambulia wazazi waliomzaa na sababu ya kumpeana kwa Betty na mumewe Mulready.

Jaji John Mativo aliyeamua kesi hiyo alisema David hakuwasilisha ushahidi wa kutosha kuthibitisha kwamba wazazi wake wa kambo walimtoa katika jumba la kuwalelea watoto wasio na wazazi la Mama Fatuma Goodwill Childrens Home.

Ilibidi Jaji Mativo kutumia sheria za kimataifa kuhusu haki za watoto kuamua kesi hiyo ya David.

David alihukumiwa kifo na aliyekuwa hakimu mkuu sasa Jaji Kiarie Waweru kwa kumnyang’anya mali kimabavu Mulready.