Habari Mseto

Korti yaelezwa Akasha alimuua mkewe, akachoma mtoto wake

July 27th, 2019 2 min read

Na BENSON MATHEKA

ALIYEKUWA mlanguzi mkuu wa dawa za kulevya Baktash Akasha anayezuiliwa Amerika, alimuua mkewe na kumchoma mwanawe kwa chuma moto, mahakama ya Amerika ilifahamishwa.

Baktash na ndugu yake Ibrahimu watasubiri kabla ya kuhukumiwa huku ikifichuliwa kuwa Baktash alielekeza ukatili aliotendea washirika wake wa biashara ya mihadarati kwa mkewe na watoto.

Katika stakabadhi ambazo waendesha mashtaka wa Amerika waliwasilisha mbele ya Jaji Morrero, Baktash alikuwa katili kupindukia hata kwa watoto na mkewe.

“Tabia ya ukatili ya Baktash haikusaza watu wa familia yake. Alitendea mkewe na mwanawe ukatili mkuu,” alieleza mahakama kwenye stakabadhi zilizowasilishwa na mwendesha mashtaka Geoffrey Berman.

Goswami 57, aliambia makachero kwamba Baktash alimtesa mwanawe kwa kumchoma kwa chuma moto. Alisema alishuhudia Baktash akimfungia mwanawe kwenye mti, akampiga bila huruma walivyokuwa wakifanyiwa watumwa enzi za zamani na kumchoma kwa chuma moto.

Wawili hawa walitarajiwa kuhukumiwa wiki hii lakini Jaji Victor Morrerro wa mahakama ya Amerika akaahirisha hukumu dhidi ya Baktash hadi Agosti 16 na Novemba 3 dhidi ya Ibrahim.

Iliibuka kuwa walikiri mashtaka baada ya kusalitiwa na mwandani wao katika biashara ya ulanguzi wa dawa za kulevya Vijaygiri Anandgiri Goswami, aliyefichulia makachero wa Amerika mienendo yao ikiwa ni pamoja na mauaji na ukatili kwa watu wa familia yao.

Raia huyo wa India alisema mtoto huyo alilazwa hospitalini akiwa na majeraha na kwa bahati nzuri alipona.

Baktash Akasha Abdalla (kushoto) na Vijaygiri Goswami awali walipofikishwa katika mahakama ya Mombasa kusikiliza kesi ambapo walihitajika Amerika. Picha/ Maktaba
Stakabadhi hizo zinafichua kwamba Baktash alimuua mkewe wa kwanza. Goswami alieleza kwamba mke wa sasa wa Baktash, Najma, alimsimulia kwamba mumewe alimuua mke wake wa kwanza.

Kulingana na Goswani, habari za Baktash kumuua mkewe zilithibitishwa wakati mmoja alipogombana na Ibrahim ambaye alimkumbusha mauaji hayo.

Baktash mwenyewe alinyamaza Ibrahim alipomkumbusha hayo.

Aidha, zinafichua kuwa Baktash pia alimpiga Najma mara kadhaa mbele ya Goswami.

Goswani alifichua hayo baada ya kukubaliana na waendesha mashtaka wa Amerika awe shahidi wao na hivyo kuwasaliti washirika wake katika biashara ya mihandarati.

Lakini licha ya ufichuzi huo, Najma ni mmoja wa watu wanaotaka Baktash aonewe huruma na mahakama.

Najma anasema kwamba maisha yake yalibadilika tangu Baktash na ndugu yake Ibrahim walipokamatwa na kupelekwa Amerika kukabiliwa na mashtaka ya kulangua dawa za kulevya.

Anaeleza kuwa maisha yamekuwa mangumu hivi kwamba analazimika kuwaoza binti zake aweze kujikimu.

Stakabadhi hizo zinaeleza jinsi wana hao walivyokuwa wakiandaa karamu baada ya kuua washindani wao katika biashara ya mihadarati katika mataifa ya kigeni.

Wamekuwa wakizuiliwa kwa miaka miwili katika jela za Amerika pamoja na Goswami na raia wa Pakistani Gulam Hussein.

Goswami na Gulam walikuwa mameneja wa mtandao wa biashara ya dawa za kulevya ya ndugu hao wa Akasha.

Mwanasiasa Stanley Livondo alitajwa kama mmoja wa washirika wa ndugu hao na ambaye wakati mmoja waligombana na wakatishia kumpiga risasi.