Habari MsetoSiasa

Korti yafanya Mutua ameze mate kukosa faini ya Sh10m za Wavinya

June 12th, 2018 1 min read

Na SAM KIPLAGAT

MBALI na kubatilisha ushindi wa Gavana wa Machakos Alfred Mutua, Mahakama ya Rufaa pia ilimkatizia shamrashamra ya kungojea faini ya Sh10 milioni kutoka kwa mshindani wake wa kisiasa Wavinya Ndeti.

Katika uamuzi wake mnamo Februari, mwaka huu, Jaji wa Mahakama Kuu Aggrey Muchelule, alitupilia mbali kesi iliyowasilishwa na Bi Ndeti na kumwagiza kulipa faini ya Sh10 milioni kwa Gavana Mutua.

Bi Ndeti aliwasilisha kesi yake katika Mahakama Kuu kupinga uchaguzi wa Dkt Mutua katika uchaguzi wa Agosti 8.

Lakini Mahakama ya Rufaa ilitupilia mbali uamuzi huo wa Mahakama Kuu na sasa ni zamu ya Gavana Mutua kumlipa Bi Ndeti kitita cha Sh2.5 milioni baada ya kushinda rufaa yake.

Katika uamuzi wao wa Ijumaa iliyopita, Majaji wa Mahakama ya Rufaa William Ouko, Mohamed Warsame na Gatembu Kairu waliagiza Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kumlipa Bi Ndeti faini ya Sh2.5 milioni.

Dkt Mutua pia aliagizwa kumlipa Bi Ndeti kiasi sawa.”Tunaagiza IEBC kuandaa uchaguzi mpya wa ugavana katoka Kaunti ya Machakos kwa mujibu wa Katiba na sheria za uchaguzi,” wakasema majaji hao baada ya kubatilisha ushindi wa Gavana Mutua.

Mbunge wa Embakasi Mashariki, Paul Ongili Babu Owino pia alinusurika kumlipa mshindani wake Bw Francis Mureithi kitita Sh2.5 milioni kwa mujibu wa uamuzi wa Mahakama Kuu uliotolewa mnamo Machi.

Badala yake Majaji wa Mahakama ya Rufaa Mohamed Warsame, Daniel Musinga na Kathurima M’Inoti waliagiza Bw Mureithi kumlipa Bw Owino faini ya Sh4 milioni.