Habari

Korti yakataa kuharamisha noti mpya

September 27th, 2019 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

WAKENYA wataendelea kutumia noti mpya za pesa zilizozinduliwa na Gavana wa Benki Kuu ya Kenya (CBK) bila kikwazo baada ya mahakama kuu kutupilia mbali kesi iliyotaka ziharamishwe.

Majaji wawili Kanyi Kimondo na Arsenath Ongeri walikubaliana kwamba noti mpya zilizozinduliwa Juni 2019 na Gavana Patrick Njoroge wakati wa sherehe ya kitaifa katika uwanja wa Narok mnamo Juni ni halali.

Lakini Jaji Antony Mrima alitofautiana nao akisema hakubaliani na wenzake kwamba pesa hizi ni halali.

Majaji Kimondo na Ongeri walisema pesa zilizo na picha ya Hayati Jomo Kenyatta ni halali kwa kuwa sheria inaikubalia.

Wakiamua kesi iliyowasilishwa na Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) Simon Mbugua na mwanaharakati Okiya Omtatah, majaji hao walisema ni CBK iliyotunukiwa jukumu la kudhibiti uchumi pamoja na uchapishaji pesa mpya.

Katika kesi hizo mbili, Mabw Mbugua na Omtatah waliomba mahakama kuu iharamishe matumizi ya pesa mpya zilizozinduliwa katika uwanja wa Narok wakati wa kusherehekea siku kuu ya Madaraka Juni 1, 2019.

Walalamishi hao walikuwa wameomba mahakama iharamishe matumizi ya pesa hizo mpya na kuamuru zile za zamani ziendelee kutumika huku CBK ikitengeneza pesa nyingine. Majaji hao walikataa ombi la kumtimua kazini Dkt Njoroge kwa kukaidi sheria kwa kutengeneza pesa zilizo na picha ya hayati Kenyatta.

“Gavana Njoroge hakukaidi sheria alipotengeneza noti mpya. Alipokea maoni kutoka kwa wananchi na mwanasheria mkuu akampa mwongozo kuhusu suala hilo,” walisema Majaji Kimondo na Ongeri.

Mbugua na Omtatah walisema watakata rufaa hapo Septemba 30, 2019, ambayo ndiyo siku ya mwisho ya kutumika kwa noti za zamani za Sh1,000.

Jaji Mrima alisema katika Kifungu nambari 231 (4) cha Katiba ya 2010 Wakenya walisema sarafu za Kenya hazifai kuwa na picha ya mtu bali alama ya kitaifa.

“Ninatofautiana na majaji wenzangu kwamba noti mpya zilizo na picha ya rais wa kwanza wa nchi hii Mzee Jomo Kenyatta ni halali,” alisema Jaji Mrima.

Picha ya Mzee Kenyatta ilipatikana kwenye noti mpya kutokana na sanamu inayopatikana karibu na jumba li mikutano la KICC jijini Nairobi.