Korti yakataa ombi kufukua aliyekufa kwa corona

Korti yakataa ombi kufukua aliyekufa kwa corona

Na DICKENS WASONGA

MAHAKAMA Kuu ya Siaya jana ilikataa ombi la familia iliyotaka mwili wa jamaa wao ufukuliwe wakisema alizikwa kama mnyama usiku wa manane baada ya kufariki kwa virusi vya corona.

Familia hiyo ilitaka mwili wa James Oyugi Onyango ambaye alikuwa mfanyakazi wa Mamlaka ya Bandari za Kenya (KPA) ufukuliwe ili ufanyiwe upasuaji kubainisha kama kweli alifariki kwa ugonjwa wa Covid-19, kisha azikwe kiheshima kwa kufuata itikadi za jamii ya Waluo.

Alizikwa usiku wa manane Aprili 12 kwenye kaburi dogo, bila jeneza.

Walalamishi wakiwemo dadaye marehemu, Bi Joan Akoth Ajuang’ na mwanawe marehemu, Bw Brian Oyugi walikuwa wameomba angalau jamaa 15 waruhusiwe kushuhudia mazishi mapya.

Katika uamuzi wake, Jaji Roseline Aburili alisema ijapokuwa ilibainika Serikali ya Kaunti ya Siaya haikufuata kanuni za Wizara ya Afya wala Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) kuhusu mazishi ya wanaokufa kwa Covid-19, itakuwa hatari kwa afya mwili huo kufukuliwa.

Alisema walalamishi hawakutoa ushahidi wowote wa kuthibitisha kama jamaa wao alifariki kutokana na ugonjwa mwingine isipokuwa Covid-19, ambao ulithibitishwa na maabara ya Taasisi ya Utafiti wa Matibabu (Kemri) mjini Kisumu.

Badala yake, aliagiza Serikali ya Kaunti ya Siaya ifanye kaburi la mwendazake kuwa nadhifu kabla siku tatu kukamilika kuanzia jana, kisha igharamie ada zote za kesi.

Ijapokuwa walalamishi waliridhishwa na uamuzi kwamba kwa kweli Kaunti ilikosea kwa jinsi ilivyomzika jamaa wao, walisikitika kuwa ombi lao la kufanya mazishi upya lilikataliwa.

Kupitia kwa wakili wao, walisema uamuzi huo utatoa mwelekeo kwa umma na serikali kuhusu hitaji la kuheshimu mazishi hata kwa walioambukizwa virusi vya corona.

You can share this post!

Mchina ndani kwa kuuza vifaa feki vya corona

Sura mbili za Raila kuhusu masaibu ya Waiguru

adminleo