Korti yakataa ombi la kukagua kura za ugavana

Korti yakataa ombi la kukagua kura za ugavana

NA PHILIP MUYANGA

MAHAKAMA Kuu imetupilia mbali ombi la kukagua na kuhesabiwa kwa kura za ugavana kaunti ya Kilifi kwenye uchaguzi mkuu uliopita.

Jaji Ann Ong’injo alisema kuwa hakukuwa na sababu mwafaka ya kuamuru kukaguliwa na kuhesabiwa kwa kura hizo.

“Nimepata ya kuwa hakuna msingi wowote umewekwa au sababu kupeanwa kwa agizo la kukaguliwa na kuhesabiwa kwa kura chini ya kifungu 82 cha sheria za kura au kanuni za uchaguzi,” alisema Jaji Ong’injo.

Bw Justin Ringa, Justin Charo na Salim Chai, ambao ni wakazi wa Kilifi wanapinga uchaguzi wa Gavana Gideon Mung’aro na naibu wake Bi Flora Chibule.

Katika uamuzi wake, Jaji Ong’injo alisema kuwa ushahidi wa maafisa watatu wa tume huru ya uchaguzi na mipaka (IEBC) ulieleza madai ya walalamishi kwa njia ambayo ilikuwa imeridhisha mahakama.

“Kwa hivyo hakuna sababu inayofanya agizo la ukaguzi na kuhesabiwa kwa kura katika vituo hivyo kutolewa,” alisema jaji Ong’injo.

Jaji huyo alisema kuwa ushahidi wa mashahidi wa walalamishi haukuridhisha mahakama kuiwezesha kutoa agizo hilo la ukaguzi na kuhesabiwa kwa kura.

Walalamishi walikuwa wamedai kulikuwa na shauku kuhusiana na kujazwa kwa makaratasi ya kupiga kura katika baadhi ya vituo vya kupigia kura.

Pia walidai kuwa kulikuwa na mambo mengi yaliyokiukwa kuhusiana na upigaji kura yakiwemo kufeli kwa chombo cha Kiems kukosa kuwatambua takriban wapiga kura 50 ambao hawakuruhusiwa kupiga kura kupitia sajili ya kura.

Mahakama ilisema kuwa mmoja wa mashahidi waliotoa ushahidi wao hawakutaja majina ya wapiga kura ambao hawakutambuliwa na chombo cha Kiems na kwamba hakuna yeyote alitoa hati ya kiapo kuonyesha kuwa hawakutambulika.

Jaji Ong’injo alisema kuwa ushahidi wa makaratasi ya kura ambayo yalikuwa yashawekwa alama katika kituo kimoja cha kupiga kura haukuwa na madai kamili kama vile nambari ya kituo na jina la mtu ambaye anadaiwa kuweka makaratasi hayo alama.

Kulingana na waweka kesi, walikuwa wameweka msingi kwa agizo la ukaguzi na kuhesabiwa tena kwa kura kwa kuwa kulikuwa na makosa yakiwemo ulaghai uliotekelezwa na IEBC.

Pia walisema kuwa mahakama ilikuwa na uwezo wa kuagiza kuhesabiwa kwa kura bila ombi lolote kufanywa na upande wowote.

Kupitia wakili Augustus Wafula, IEBC iliambia mahakama hakuna shahidi yeyote wa walioshtaki alitaja kituo kamili cha kupiga kura ambacho kilikuwa na dosari ili kuwezesha agizo hilo la kukaguliwa na kuhesabu kura litolewe.

Bw Wafula aliiambia mahakama ya kuwa mashahidi wa waweka kesi hawakutoa ushahidi wowote wa mambo ambayo hayakufanyika vizuri ambao ungesemekana kuathiri au ungeathiri majibu yaliyotolewa na IEBC.

Mahakama inatarajiwa kutoa uamuzi wa kesi hiyo ya uchaguzi mnamo Februari 16.

  • Tags

You can share this post!

MALEZI KIDIJITALI: Likizo ya dijitali hutuliza watoto

Ruto anavyomfufua Uhuru kisiasa

T L