Korti yapatia serikali kibali kutwaa jumba la aliyeuawa

Korti yapatia serikali kibali kutwaa jumba la aliyeuawa

Na RICHARD MUNGUTI

SERIKALI imetwaa jumba lililojengwa kwa fedha za kundi la wapiganaji wa al-Shabaab jijini Nairobi.

Jumba hilo lililoko katika eneo la Nasra Gardens Estate, mtaani Umoja III, lilijengwa na Anwar Yogan Mwok ambaye alikuwa akipokea fedha kutoka kwa kundi hilo la wapiganaji.

Mwok aliuawa mnamo 2017 katika makabiliano makali na wanajeshi wa KDF nchini Somalia.

Kulingana na ushahidi uliowasilishwa kortini, Mwok alikuwa akikusanya kodi kutoka kwenye jumba hilo na kutuma hela kwa al-Shabaab.

Jumba hilo lilikuwa likisimamiwa na mama ya Mwok, Bi Rose Awinja Ondumbu, ambaye mahakama jana iliagiza awekwe chini ya usimamizi wa polisi kwa miaka mitano.

Jumba hilo lilikuwa limekodishiwa diwani wa Kaunti ya Machakos tangu 2017.

Bi Awinja alijihusisha na usimamizi wa jumba hilo kati ya Desemba 1, 2013 na Machi 15, 2017.

Hakimu mwandamizi Bw Kenneth Cheruiyot Mwok alimpata na hatia Bi Awinja kwa kumiliki na kukodisha mali iliyostawishwa kwa pesa za kundi la kigaidi la al-Shabaab.

Hakimu alisema sheria imesema ikiwa imethibitishwa mali imestawishwa na fedha za kundi la kigaidi litwaliwe na serikali.

Hakimu alisema upande wa mashtaka ulioongozwa na wakili wa serikali.

“Hii mahakama imechambua na kuzingatia ushahidi wote uliowasilishwa na upande wa mashtaka na kufikia uamuzi Awinja yuko na hatia ya kusimamia na kupokea pesa kutoka kwa jumba la gaidi wa al-Shabaab,” alisema Bw Cheruiyot.

Hata hivyo hakimu alifutilia mbali shtaka Awinja kutuma pesa kwa kundi hilo la al-Shabaab kutokana na ada ya kukodishwa kwa jumba hilo.

Akiomba mahakama imwonee huruma wakati wa kupitisha adhabu, Awinja alisema hakujua mwanawe alikuwa gaidi kwani alimweleza aliajiriwa nchini Somali na shirika moja la kimataifa.

Awinja alieleza korti kwamba alifahamishwa kuwa mwanawe ni gaidi alipouawa na maafisa wa KDF.

Punde tu baada ya habari kuenea Mwok alikuwa gaidi, mkewe na mwanawe walitoroka na kumwacha mshtakiwa peke yake akiugua huku uzee ukimkaba kabisa.

“Naomba hii mahakama inioneee huruma kwa vile mimi sina mbele wala nyuma. Mwanangu aliuawa Somalia. Mkewe alitoroka na mjukuu wangu. Nimesalia pweke na mgonjwa.Uzee nao umebisha kwa kasi,” Awinja alimrai hakimu.

Mahakama iliombwa na wakili John Khaminwa ambaye alikuwa mahakamani imwonee huruma Awinja anayeugua na mwili wake umedhoofika.Akipitisha hukumu hakimu alisema, “Hii mahakama imetilia maanani wewe humgojwa na hauna mtu wa kukutunza. Kukupeleka jena miaka 20 au zaidi ni sawa na kupitisha adhabu ya kifo dhidi yako.”

Hatimaye aliagizwa awe chini ya uangalizi wa polisi kwa miaka mitano.

Kesi hiyo itatajwa tena Desemba 16, 2021 kwa maagizo zaidi.

You can share this post!

EACC yammulika gavana wa Lamu

Omanyala sasa ni Inspekta wa Polisi, atawakilisha idara...

T L