Habari Mseto

Korti yaruhusu LSK kuandamana kuhusu Bunge

October 9th, 2020 2 min read

Na WAANDISHI WETU

MAHAKAMA Kuu imekataa ombi la kuzuia Chama cha Mawakili nchini (LSK) kuandamana katika majengo ya bunge kumshinikiza Rais Uhuru Kenyatta kuvunja bunge.

LSK ilimpatia Rais Kenyatta hadi Oktoba 12 avunje bunge kwa kushindwa kutunga sheria ya kuhakikisha usawa wa jinsia alivyoshauri Jaji Mkuu David Maraga.

Jaji Weldon Korir alisema mawakili hawawezi kuzuiwa kutekeleza haki yao ya kuandamana mradi tu wafanye hivyo kwa kuzingatia sheria.

Bunge la Kitaifa na lile la Seneti liliwasilisha ombi wakati wa kusikizwa kwa kesi ilyowasilishwa baada ya ushauri wa Jaji Maraga wa kuvunjwa kwa bunge.

Akikataa ombi la mabunge hayo mawili la kuzuia maandamano hayo yenye kauli mbiu ‘Kaa Bunge’, Jaji huyo alisema hawezi kutoa amri kwa asasi au mtu yeyote ambaye hahusiki na kesi hiyo.

LSK inapanga maandamano kuanzia Jumatatu wiki ijayo kama njia ya kumshinikiza Rais Kenyatta atekeleze ushauri wa Bw Maraga.

Mwenyekiti wa LSK, Nelson Havi amekuwa akishikilia kwamba, Rais Kenyatta hana budi ila kukumbatia ushauri wa Jaji Mkuu huku pia akiitaka Wizara ya Usalama wa Ndani iwaondoe walinzi wote wa wabunge na maseneta.

“Tutafanya maandamano hayo kwa kuzingatia sheria. Tunawakaribisha Wakenya ambao pia wanataka kupigania haki yao kwa kufuata sheria,” akasema Bw Havi.

Na jana, maafisa wa Chama cha UGM, wakiongozwa na aliyekuwa Naibu Gavana wa Nairobi Jonathan Mueke na mbunge wa zamani wa Ndhiwa, Agostino Neto walijiunga na LSK kuwashawishi Wakenya waungane nao kumshinikiza Rais avunje bunge.

“Bunge hili limekuwa kitovu cha kuwabagua wanawake, vijana, walemavu, watoto na wakongwe. Wakenya lazima wajitokeze ili wahakikishe wanashinda vita dhidi ya ukosefu wa usawa. Ndiyo maana bunge hili lazima livunjwe. Uhuru haupatikani k wa urahisi, lazima upiganiwe,” akasema Bw Mueke.

Hata hivyo, Jaji Mkuu Maraga bado hajabuni jopo la majaji watatu kusikiza na kuamua kesi iliyowasilishwa mahakamani kuhusiana na ushauri wake ambao umezua maoni mseto miongoni mwa wabunge na maseneta.

Jaji Weldon Korir alisema hakuwa amepata taarifa zozote kutoka kwa Jaji Maraga wakati wa kutoa mwelekeo kuhusu kesi hiyo jana.

“Iwapo kuna jopo, basi mawakili watajulishwa,” akasema Jaji Korir.

Aliamuru kesi hiyo itajwe Oktoba 21, 2020, kwa mwelekeo zaidi na pia ithibitishwe iwapo Jaji Mkuu atakuwa amebuni jopo kufikia wakatu huo. Pia aliongeza muda wa amri inayomzuia Rais Kenyatta kuvunja bunge hadi suala hilo lisikizwe na kuamuliwa na korti.

Wakati huo huo, mashirika ya kutetea haki za wanawake yamesema yatajiunga na mawakili kuandamana katika majengo ya bunge wiki ijayo iwapo Rais hatatekeleza ushauri wa Bw Maraga.

Akihojiwa na runinga ya France 24, akiwa Ufaransa wiki jana, Rais Kenyatta alisema hana nia ya kuvunja bunge kwa sasa ingawa alisema suala hilo bado limo mahakamani.