Habari Mseto

Korti yaruhusu NCIC na Kuria kusuluhisha kesi ya uchochezi

April 19th, 2018 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA imemkubalia Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria kuendelea na mashauriano pamoja na Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC) ya kutamatisha kesi ya chuki na uchochezi aliyoshtakiwa.

Hakimu mkuu katika mahakama ya Milimani Nairobi Bw Francis Andayi alielezwa “bado suluhu haijafikiwa katika mazugumzo kati ya Bw Kuria na NCIC inayoongozwa na Spika wa zamani kwenye bunge la kitaifa Bw Francis ole Kaparo kuhusu kuondolewa kwa kesi inayomkabili mwanasiasa huyu ya uchochezi.”

Bw Andayi aliombwa apatie pande zote muda zaidi zijadiliane na kufikia suluhu.

“Katiba inakubalia njia mbadala ya kusuluhisha mizozo kwa kuwakubalia wanaozozana kushauriana kwa lengo la kutafuta suluhu,” Bw Andayi alifahamishwa.

Bw Andayi alifahamishwa kwamba mashauri kati ya Bw Kuria na NCIC yakikamilika “ripoti itawalishwa kortini na uamuzi wa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Bw Noordin Haji utatolewa mahakamani.”

Korti iliombwa itaje kesi hiyo dhidi ya Bw Kuria mnamo Mei 29 2018 ndipo kiongozi wa mashtaka Bw Solomon Naulikha na wakili wa mshtakiwa waeleze iwapo wahusika wameafikiana.

Bw Kuria anakabiliwa na shtaka la kutumia lugha chafu na ya matusi dhidi ya kinara wa Nasa Bw Raila Odinga na mkewe Bi Aida mnamo Septemba 5, 2017.

Bw Kuria anadaiwa alimtukana Bw Odinga katika soko la Wagige iliyoko eneo la Kikuyu kaunti ya Kiambu.

Shtaka linasema maneno aliyotumia Bw Kuria yalilenga kumjeruhi Bw Odinga. Pia anadaiwa alimkejeli mkewe waziri huyu mkuu wa zamani.

Bw Andayi alikubalia ombi la kuzipa pande zote muda wa kushauriana akisema, “Katiba inakubalia wanaozozana kutafuta suluhu nje ya mahakama almaafuru ADR.”

Kesi hiyo itatajwa tena mnamo Mei 29, 2018.