Habari Mseto

Korti yasitisha kesi ya wakurugenzi wa bwawa la Solai

January 15th, 2020 1 min read

Na Richard Munguti

HAKIMU mkuu mahakama ya Makadara Bw Eston Nyaga amesitisha kusikizwa kwa kesi ya ulaghai wa shamba la Sh2 bilioni inayowakabili wakurugenzi wawili wa kampuni ya Kensalt Limited iliyostawisha bwawa la Solai iliyoko kaunti ya Nakuru.

Mwaka wa 2018 bwawa hilo lilivunja kingo zake na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 40.

Akisitisha kusikizwa kwa kesi dhidi ya Mabw Mansukhulal Patel na Perry Mansukh Kasangra Bw Nyaga alisema “lazima maagizo ya mahakama kuu yafuatwe.”

“ Hii mahakama iliagizwa na Jaji Pauline Nyamweya isitishe kusikizwa kwa kesi dhidi ya Patel na Kasangra.Sina budi kuitii agizo hili,” alisema Bw Nyaga.

Patel,Kasangra na Mbunge wa zamani Baringo kusini Lawi Kigem Kiplagat wameshtakiwa kula njama kumpora aliyekuwa Mbunge wa Lamu Mashariki Abubakar Madhubuti shamba hilo la ekari 10 katika eneo la Kia Ng’ombe Embakasi Nairobi kati ya 1986 na 1996.

Bw Nyaga alisema mahakama kuu iliamuru kesi iliyowasilishwa na Mabw Patel, Kasangra na aliyekuwa Mbunge wa Baringo kusini Lawi Kiplagat isikizwe katika muda wa siku 21.

Aliamuru kesi hiyo itajwe Machi 9, 2020.

“Kwa vile Patel na Kasangra hawajajibu mashtaka basi ni Kiplagat na James Wainaina Ndung’u wataofika kortini Machi 9, 2020,” alisema Bw Nyaga.

Mnamo Desemba 27 2019 Jaji Nyamweya alisitisha kesi waliyoshtakiwa Patel, Kasangra na Kiplagat.

Wakili William Arusei aliyeiwasilisha ombi hilo alisema polisi wamekaidi agizo la Mahakama kuu kuwashtaki wanne hao Patel, Kasangra , Kiplagat na Wainaina iliyowataka wanaodai umiliki wa shamba hilo wasiliingilie kulistawisha hadi mwenyewe ajulikane.