Habari

Korti yasitisha kuongezwa kwa ada ya kuegesha magari jijini Nairobi

December 30th, 2019 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA Kuu Jumatatu imeamuru serikali ya Kaunti ya Nairobi isiongeze ada ya kuegesha magari hadi kesi iliyowasilishwa na shirikisho la watumiaji bidhaa (Cofek) isikizwe na kuamuliwa.

Jaji James Makau aliamuru kesi iliyowasilishwa na Cofek isikizwe Februari 17, 2020.

Jaji Makau aliiamuru serikali ya kaunti ya Nairobi iendelee kutoza ada za zamani kwa magari yote hadi kesi iliyowasilishwa na Cofek isikizwe na kuamuliwa.

Jaji Makau alisema , kesi hiyo ingelisikizwa Januari 2020 lakini anasikiza kesi nyingine katika mahakama kuu pamoja na majaji wengine wawili zinazohusu masuala ya katiba.

“Naamuru maombi ya kupinga kesi hii yaliyowasilishwa na kaunti ya Nairobi kupitia kwa wakili Harrisson Kinyanjui yaondolewe ndipo kesi hii iweze kusikizwa na kuamuliwa kwa upesi,” alisema Jaji Makau.

Akiwasilisha kesi ya Cofek, wakili Henry Kurauka, ameeleza mahakama kwamba wakazi wa Nairobi hawakuarifiwa kama inavyotakiwa kisheria kabla ya kuongeza ada za magari ya wamiliki binafsi na ya kibiashara.

Ada ya kuegesha gari dogo iliongezwa kutoka Sh200 hadi Sh400.