Kimataifa

Korti yatoa mwanya kwa Museveni kutawala maisha

July 30th, 2018 2 min read

Na AFP

RAIS Yoweri Museveni wa Uganda anaelekea kuwa rais wa maisha baada ya mahakama kuidhinisha mabadiliko ya kikatiba ya kuondoa kipengele cha umri wa juu unaohitajika kwa wagombeaji urais.

Kabla ya katiba kubadilishwa, rais alipaswa kuwa na umri wa chini ya miaka 75, hitaji ambalo lingemzuia Museveni, ambaye ameongoza nchi hiyo tangu 1986, kugombea urais kwenye uchaguzi wa 2021.

Mswada uliowasilishwa bungeni Septemba mwaka jana na kutiwa sahihi kuwa sheria Desemba mwaka huo ulizua maandamano na lawama kutoka kwa upinzani, ambao unamlaumu Museveni kwa kukatalia mamlakani.

Kundi la viongozi wa upinzani liliwasilisha kesi katika mahakama ya kikatiba iliyoamuliwa Alhamisi wiki jana na mabadiliko hayo kuidhinishwa.

“Mahakama imekubali rais wa maisha,” alisema wakili Ladislaus Rwakafuzi ambaye ni mtetezi wa haki za binadamu.

“Nafikiri majaji wetu walikosa ujasiri wa kumwambia Rais kwamba amekuwa mzee na wakati wake wa kuondoka umefika,” aliongeza.

Majaji wengi wa mahakama ya kikatiba waliotoa uamuzi wao kutoka mji wa Mbale, ulio kilomita 225 mashariki ya Kampala, waliunga mknono kuondolewa kwa umri wa juu wa wanaogombea urais.

Wakili Rwakafuzi aliwakilisha muungano wa upinzani unaotaka hitaji la umri wa wagombeaji lirejeshwe.

Rwakafuzi aliongeza kwamba atashauriana na wateja wake kubaini iwapo watakata rufaa.

Kiongozi wa upinzani bungeni, Winnie Kiiza alisema wanaweza kupata haki katika kiwango kingine.

Lakini majaji walikataa juhudi za wabunge za kuongeza vipindi vyao vya kuhudumu kutoka miaka mitano hadi saba, hatua ambayo ingesongesha uchaguzi hadi 2023 huku mmoja wa majaji akitaja hatua hiyo kuwa ya ubinafsi.

Majaji hao pia waliamua kwamba juhudi za kurejesha vipindi vya rais kuhudumu ambavyo viliondolewa siasa za vyama vingi ziliporejeshwa 2005 katiba ilipobadilishwa mara ya mwisho, ni ukiukaji wa mfumo wa bunge.

Waliamua kwamba juhudi hizo hazina msingi wa kisheria na kutoa nafasi kwa Museveni kutawala maisha.

Museveni, ambaye alitwaa uongozi akiwa kingozi wa waasi 1986 aliwahi kunukuliwa akisema kwamba viongozi wanaokatalia mamlakani ndio chanzo cha matatizo barani Afrika.

Hata hivyo, alipokuwa akigombea kwa kipindi cha tano mnamo 2016, alisema wakati wake wa kuondoka mamlakani haujafika kwa sababu angali na kazi nyingi ya kufanya.

Naibu Mwanasheria Mkuu Mwesigya Rukutana, ambaye aliwakilisha serikali katika kesi hiyo alisema alifurahia uamuzi huo.