Habari Mseto

Korti yazima mawakili waliopinga NMG ikiripoti kesi ya NYS

November 2nd, 2018 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MAGAZETI ya Taifa Leo, Daily Nation, Business Daily na The East African yanayochapishwa kampuni ya Nation Media Group yataendelea kuchapisha na kutangaza ushahidi katika kesi ya sakata iliyokumba shirika la NYS na kupelekea kupotea kwa zaidi ya Sh11 bilioni.

Hakimu mkuu Bw Douglas Ogoti anayesikiza kesi hiyo alikataa kujiondoa kusikiza kesi dhidi ya waliokuwa maafisa wakuu wa NYS , wafanyabiashara na aliyekuwa katibu katika Wizara ya Michezo na Jinsia Bi Lilian Mbogo Omollo.

Bw Ogoti alikuwa ameombwa na mawakili wanaowakilisha washukiwa 37 wanaokabiliwa na mashtaka 37 azuie magazeti hayo yasichapishe habari kuhusu kesi hiyo ya kashfa ya NYS wakidai yanapotosha na kutweza ukweli.

Hata hivyo Bw Ogoti alisema, “nimesoma na kuelewa habari zinazolalamikiwa lakini haziwezi kumpotosha msomaji.”

Hakimu alikubalia magazeti haya yaendelee na kazi yao lakini akatahadharisha waandishi wa vyombo vya habari wasipotoshe katika  utendakazi wao.

Aliamuru kesi iendelee na afisa mkuu kutoka Wizara ya Ugatuzi Bw Sebastian John Mouko akaendelea kutoa ushahidi.

Bw Mouko alieleza mahakama kuwa kampuni 36 ziliwasilisha maombi ya kutoa huduma kwa NYS.

Alisema kampuni moja ijulikanayo kama Jiwaco ilikuwa inauzia NYS maharagwe yaliyowekwa ndani ya mikebe na kulipwa Sh6 milioni.

Kesi inaendelea.