Korti yazima serikali kuagiza mahindi tata

Korti yazima serikali kuagiza mahindi tata

NA LEONARD ONYANGO

MAHAKAMA imepiga breki mpango wa serikali ya Rais William Ruto wa kuagiza magunia milioni 10 ya mahindi yaliyobadilishwa maumbile (GMO).

Jaji Thande Mugure wa Mahakama Kuu pia amewazima mawaziri Moses Kuria (Biashara) na Mithika Linturi (Kilimo) kuchapisha kwenye Gazeti Rasmi la Serikali taarifa ya kuruhusu wafanyabiashara kuleta humu nchini mahindi ya GMO, hadi pale kesi hiyo itakaposikilizwa na kuamuliwa.

Uamuzi wa mahakama umetokea wakati ambao mawaziri wanaonekana kutofautiana kuhusu suala la mahindi ya GMO, kufuatia tangazo la mpango huo lililotolewa na Bw Kuria.

Jana Jumatatu, Kinara wa Mawaziri, Musalia Mudavadi alitofautiana vikali na Bw Kuria kuhusu uagizaji wa mahindi hayo, akisema kuwa suala la uagizaji wa mahindi ya GMO linafaa kushughulikiwa na Wizara ya Kilimo na wala si Wizara ya Biashara.

“Suala la uagizaji wa mahindi linafaa kushughulikiwa na Wizara ya Kilimo. Wizara hiyo ndiyo inafaa kujua ni kiasi kipi cha mahindi kinafaa kuagizwa kutoka nje,” akasema Bw Mudavadi.

Hatua ya Bw Mudavadi kujitenga na Bw Kuria imeibua maswali zaidi kuhusu anayelenga kunufaika na biashara na mahindi ya GMO. Kati ya maswali hayo ni: Ni kwa nini Bw Linturi ametengwa katika suala la uagizaji wa GMO; Bw Kuria anapigania masilahi ya nani? Ni kwa nini Bw Kuria alitangaza mpango wa kutaka kuagiza mahindi ya GMO bila idhini ya Baraza la Mawaziri?

Wikendi, Bw Kuria aliongeza juhudi za kuhakikisha mahindi ya GMO yameagizwa alipowapa wakulima makataa ya saa 72 kuuza mahindi waliyohifadhi ghalani kabla ya wafanyabiashara kuruhusiwa kuanza kuleta mahindi ya GMO.

Bw Kuria alishutumu wakulima kwa madai ya kuficha mazao hayo wakingojea kuyauza kwa bei ya juu ilhali mamilioni ya Wakenya wanahangaishwa na njaa.

“Mamilioni ya Wakenya wanahangaishwa na njaa kwa sababu wakulima wamemua kuficha mahindi yao ghalani. Wanangoja kuyauza kwa bei ya juu. Wakulima wana hadi Jumanne kuuza,” akasema Bw Kuria.

Lakini jana Jumatatu, Bw Linturi alitofautiana na Bw Kuria akisema kuwa serikali haiwezi kulazimisha wakulima kuuza mahindi yao kwa vitisho.

“Serikali haiwezi kulazimisha wakulima kuuza mahindi yao. Nawasihi wakulima walio na mahindi ya ziada wasiuze kila kitu, mbali waache kiasi kidogo cha kutumia,” akasema Bw Linturi alipokuwa akizungumza katika Jumba la Kilimo alipokutana na Baraza la Magavana.

Mpango huo wa kuagiza mahindi ya GMO umemtia motoni Bw Kuria baada ya viongozi kutoka maeneo ya Magharibi na Bonde la Ufa kutishia kumtimua. Hata hivyo, Rais Ruto aliingilia kati na kuwazima.

HATARI

Kwa upande wake, upinzani ukiongozwa na Raila Odinga ulidai kuwa mahindi ya GMO ni hatari kwa afya na kutaka serikali kushauriana na Wakenya kabla ya kuruhusu mahindi hayo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Kuhakiki Usalama wa Vyakula au Mimea iliyobadilishwa Maumbile (NBA), Dkt Roy Mugiira jana aliambia Taifa Leo kuwa mamlaka hiyo haijapokea maombi yoyote kutoka kwa wafanyabiashara wanaolenga kuleta mahindi ya GMO nchini.

Kesi ambayo imepelekea kusitishwa kwa mpango Bw Kuria iliwasilishwa kortini na vuguvugu la kutetea wakulima wa mashamba madogo linalotaka serikali kutupilia mbali mpango wake wa kuleta mahindi ya GMO.

Hiyo ni kesi ya pili ambayo imewasilishwa kortini kupinga mpango huo wa mahindi hayo. Vuguvugu hilo linadai kuwa utaratibu uliotumiwa na serikali ya Rais Ruto kuondoa marufuku iliyowekwa mnamo 2012 na serikali ya Mwai Kibaki dhidi ya GMO ulikiuka sheria. Vuguvugu hilo linadai kuwa mahindi ya GMO ni hatari kwa afya.

Kesi nyingine ya kupinga GMO iliwasilishwa kortini na Paul Mwangi, anayedai kuwa uamuzi wa kuondoa marufuku dhidi ya mahindi hayo uliharakishwa.

Kulingana na Bw Mwangi, uamuzi huo wa serikali ni hatari kwa wakulima wa mashamba madogo.

You can share this post!

Watahiniwa wahamishwa kwa ndege ya KDF msituni Boni

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Ghana walima Korea Kusini na...

T L