K’Osewe alidai nilichovya asali ya mkewe, mshtakiwa wa jaribio la mauaji afichua kortini

K’Osewe alidai nilichovya asali ya mkewe, mshtakiwa wa jaribio la mauaji afichua kortini

Na RICHARD MUNGUTI

AFISA wa mauzo katika kampuni moja ya utalii alijipata taabani kutokana na kinywa chake kilichojaa matusi na majivuno Jumatatu aliposukumwa jela kwa kumwita mmiliki wa hoteli moja maarufu jijini Nairobi ‘mnyama’ ndani ya mahakama.

Tom Oywa Mboya ambaye kilio chake kwamba amepokea simu mtu wa familia yake ameaga dunia hakikusikika alitiwa pingu haraka haraka na kusukumwa jela mara moja.

“Ukiwa jela utafikiria vyema lugha utakayokuwa unatumia ndani na nje ya mahakama. Siwezi kuruhusu mtu yeyote kumdunisha binadamu mwenzake kwa kumwita majina ya wanyama wa mwituni. Sio kwa hii korti yangu. Ikiwa nawaheshimu binadamu wenzangu, sembuse wewe?” hakimu Martha Mutuku alaimuru wa mahakama ya Milimani.

Mboya alikuwa ameonywa mara kadha na Bi Mutuku dhidi ya kutumia lugha chafu na kumdunisha William K’Osewe Guda , mmiliki wa hoteli ya Ronalo Kosewe, Nairobi maarufu kwa maankuli ya samaki.

Mboya ambaye Desemba 1, 2016 alijaribu kumuua K’Osewe kwa kumpiga risasi alikuwa akijitetea baada ya kupatikana na kesi ya kujibu.

Akitoa ushahidi aliulizwa na kiongozi wa mashtaka Bw Anderson Gikunda ikiwa K’Osewe alishtuka baada ya kusikia milio ya risasi.

Mboya alijibu, “Alishtuka kisha akalala chini akinikaripia. Huyu ni mnyama mwitu. Mnyama huyu kabisa.”

Wakati huo mahakama ilimuonya mshtakiwa dhidi ya kutumia lugha chafu lakini “sikio la kufa halihisi dawa. Aliendelea kuchemka kwa hasira huku akimkondolea macho K’Osewe aliyekuwa ameketi kortini ameshika mkokonjo.”

Bw K’Osewe alicheka na kueleza mahakama “huyu mshtakiwa ananichukia zaidi.”

Bw K’Osewe wakati wa kesi Januari 19, 2021. PICHA/ RICHARD MUNGUTI

“Unasikia anavyoniita?” K’Osewe alisema kwa sauti akiongeza, “alinipiga risasi ya mgongo na kuniumiza. Siwezi kutembea kama zamani.”

Mahakama ilimtaka Guda anyamaze sheria ishike mkondo wake. Mboya alihukumiwa kusukumwa jela siku moja awaze na kuwazua kuhusu matamshi na lugha yake kwa binadamu aliokumbushwa sio ayawani.

Ameshtakiwa kujaribu kumuua William K’Osewe Guda mnamo Desemba 1 2016 katika eneo la Garden Estate.

Wakili anayemwakilisha Bw Mboya alijaribu kuingilia kati kuomba msamaha kwa kumtetea lakini hakufanikiwa.

Bw Mboya alisema alimpiga risasi Bw K’Osewe kwa vile alikuwa ametisha kumshambulia mara kadha akidai alikuwa amelala mara kadha na mkewe.

“Nilikuwa natoka kula maankuli ya mchana katika hoteli ijulikanano Hagon iliyoko Garden Estate. Bw Osewe alinizuia kwa gari lake kisha akaniambia nitaona cha mtema kuni kwa vile nimekuwa nikilala na mkewe,” Bw Mboya alijitetea.

Alisema alifyatua risasi mbili angani amshtue Bw K’Osewe lakini aliendelea kumsongea akimwelekezea bastola.

“Nilimpiga risasi ya mkono ndipo aachilie bastola yake,” mshtakiwa alimweleza Bi Mutuku.

Alikana alimpiga risasi ya mgongo Bw K’Osewe “Ulinipiga risasi ya mgongo. Niko hapa kortini natembea kwa mikogonjo. Wacha kudanganya korti,” Bw Osewe alipaasa sauti na kumweleza hakimu.

Mshtakiwa alisema K’Osewe alijaribu mara mbili kufyatua bastola lakini risasi zikakwama kutoka.

You can share this post!

Tangatanga watimua wahubiri na kuteka mazishi ya diwani

Wanasiasa wanaofadhili ghasia Kapedo kukamatwa