Michezo

Kosgei atiwa kwenye orodha ya wanariadha watakaonogesha mbio za Delhi Half Marathon

November 24th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

MSHIKILIZI wa rekodi ya dunia katika marathon, Brigid Kosgei ametiwa katika orodha ya washiriki wa kike watakaonogesha mbio za Airtel Delhi Half Marathon (ADHM) mnamo Novemba 29, 2020.

Hatua hiyo inafanya makala ya 16 ya kivumbi hicho cha World Athletics Label kuwa chenye ushindani mkali zaidi katika historia na miongoni mwa mbio ambazo zitajumuisha wanariadha wa haiba kubwa zaidi mwaka huu.

Japo Kosgei anapigiwa upatu wa kuibuka mshindi wa mbio hizo, atatolewa kijasho na Mwethiopia Ababel Yeshaneh.

Wakati wa mbio za Chicago Marathon mnamo Oktoba 2019, Kosgei aliduwaza wengi alipofika utepeni baada ya muda wa saa 2:14:04 na kuvunja rekodi ya dunia kwa zaidi ya dakika moja. Yeshaneh aliambulia nafasi ya pili katika kivumbi hicho kwa saa 2:20:51

Ingawa hivyo, Yeshaneh alilipiza kisasi dhidi ya Kosgei katika mbio za Ras Al Khaimah Half Marathon mnamo Februari mwaka huu. Alitamalaki kivumbi hicho kwa saa 1:04:31 huku Kosgei akiridhika na nafasi ya pili (1:04:49).

Katika mbio za hivi karibuni zaidi ambazo wawili hao walishiriki mnamo Oktoba, Kosgei, 26, aliibuka mshindi wa London Marathon (2:18:58) huku Yeshaneh, 29, akiambulia nafasi ya tano baada ya kuanguka zikisalia kilomita tatu pekee kwenye Nusu Marathon ya Dunia iliyoandaliwa jijini Gdynia, Poland.

Mwethiopia Tsehay Gemechu ambaye ni mshikilizi wa rekodi ya New Delhi Half Marathon atakuwa akipania kutetea ubingwa wake na kuibuka mshindi wa mbio hizo kwa mara ya tatu mfululizo. Mnamo 2019, Gemechu aliimarisha rekodi yake kwenye mbio hizo kwa kupunguza zaidi ya sekunde 50 alipokata utepe baada ya saa 1:06:00.

Mbali na Yeshaneh na Gemechu, Waethiopia wengine wanaotarajiwa kuwa mwiba mkali kwa Kosgei na washindani wengine kwenye mbio za Novemba 29 uwanjani Jawaharlal Nehru ni Yalemzerf Yehualaw na Netsanet Gudeta.

Yehualaw aliyeridhika na nafasi ya tatu nchini Poland (saa 1:05:19), aliambulia nafasi ya pili kwenye mbio za ADHM mnamo 2019 baada ya Gemechu kumpiku kwa sekunde moja pekee. Gudeta aliyeibuka bingwa wa Nusu Marathon ya Dunia mnamo 2018, alitupwa hadi nafasi ya nane nchini Poland mwezi Oktoba.

Shirikisho la Riadha Duniani (WA) limetenga jumla ya Sh23 milioni kutuza washiriki wa mbio hizo za ADHM huku washindi wa kila kitengo kwa upande wa wanawake na wanaume akitia kapuni Sh2.7 milioni.

Wiki chache baada ya kuambulia pakavu kwenye Nusu Marathon ya Dunia jijini Gdynia, mshindi wa zamani wa nishani ya fedha katika mbio za nyika barani Afrika, Leonard Barsoton atakuwa tegemeo la Kenya kwenye ADHM.

Barsoton alitupwa hadi nafasi ya sita kwenye Nusu Marathon ya Dunia iliyotawaliwa na Mganda Jacob Kiplimo jijini Gdynia. Mkenya Kibiwott Kandie aliambulia nafasi ya pili.

Barsoton amesema maazimio yake kwenye mbio za New Delhi hayatakuwa tu kutwaa nishani ya dhahabu, bali pia kuboresha zaidi muda wake binafsi wa dakika 59:09 kwenye mbio za kilomita 21.

“Nina malengo mapya ambayo sina shaka kwamba yatazaa matunda wakati wa kivumbi cha New Delhi. Niko tayari kwa kibarua hicho kwa kuwa nimejiandaa vya kutosha,” akasema Barsoton.

Mbio za New Delhi litakuwa shindano la tatu kwa Barsoton kushiriki mwaka huu baada ya kuambulia pia katika nafasi ya sita kwenye kivumbi cha Ras Al Khaimah (RAK) Half Marathon kisha kutwaa ubingwa wa mbio za kilomita 25 barabarani za Kolkota. Katika mbio hizo za Kolkota, Barsoton alisajili muda wa dakika 63:05 na kuvunja rekodi ya Mwethiopia Kennenisa Bekele.

Barsoton, ambaye pia ni bingwa wa Michezo ya Afrika katika mita 10,000, amesema kwamba hatishwi na hali mbovu ya hewa – ya upepo mkubwa kwa sasa mjini New Delhi, India.

Barsoton atatoana jasho na Wakenya Josphat Boit (59:19) na Edwin Kiptoo (59:26). Mbio hizo za New Delhi Half Marathon zimevutia pia wanariadha Abraham Cheroben (Bahrain) pamoja na waethiopia Guye Adola, Amdework Walelegn, Andamlak Belihu na Solomon Berihu.