Michezo

KPA na GSU wazidi kufana voliboli

June 24th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

WAFALME wa voliboli nchini, Kenya General Service Unit (GSU) na Halmashauri ya Bandari ya Kenya (KPA) kila moja ilivuna alama sita muhimu kwenye mechi za Ligi Kuu ya KVF msimu huu zilizochezewa mjini Voi, Kaunti ya Taita Taveta.

Wanaume wa GSU waliipepeta Western Prisons seti 3-0 (25-10, 25-11, 25-22) kisha kuzoa seti 3-0(25-11,25-17,25-20) dhidi ya Vihiga County.

Nao madume wa KPA walibeba ufanisi wa mechi mbili kwa seti 3-1 kila moja mbele ya Vihiga County na Prisons Mombasa.

Nayo Kenya Prisons ilinyanyua wenzao wa Western Prisons kwa seti 3-0 huku Mombasa Prisons ikitandika Nairobi Prisons seti 3-0 (25-21, 25-18, 25-19).

Nao malkia wa mchezo nchini, Kenya Prisons ilikomoa Ashton seti 3-0 huku vipusa wa KCB wakiandikisha ushindi wa seti 3-0 (25-11, 25-21, 25-13) mbele ya DCI.

Kufuatia matokeo hayo, wanaume wa Halmashauri ya Bandari ya Kenya (KPA) na vipusa wa Kenya Prisons kila moja imeongoza kwenye jedwali ya kipute hicho kukusanya alama 15 na sita mtawalia.

Kikosi cha GSU kinashikilia nafasi ya pili kwa kuzoa alama 12, sawa na Wanajeshi wa Ulinzi (KDF) pia Administration Police of Kenya (AP Kenya) tofauti ikiwa idadi ya seti.

Nao warembo wa KCB ambao hunolewa na kocha, Japheth Munala awali akifundisha Kenya Pipeline wamekamata nafasi ya pili kwa alama sita nayo DCI inafunga tatu bora ikiwa na alama tatu sawa Kenya Pipeline tofauti ikiwa idadi ya seti.