Habari Mseto

KPC yawekeza Sh1.4 bilioni kukabiliana na majanga 

April 15th, 2024 1 min read

NA TITUS OMINDE

KAMPUNI ya Kenya Pipeline imewekeza kima cha Sh1.4 bilioni katika uboreshaji wa kisasa wa Taasisi ya Mafuta na Gesi ya Morendat ili kuimarisha mafunzo ya kudhibiti majanga. 

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo, Gabriel Chege alisema wameshirikiana na mashirika mbalimbali ya serikali na yale ya kibinafsi kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wao kuhusu mbinu za kukabiliana na mikasa mbalimbali kama vile moto, mafuriko miongoni mwa majanga mengine.

“Tumeshirikiana na mashirika ya serikali na ya misaada ya kibinadamu kote nchini kutoa mafunzo kuhusu mbinu salama za kukabiliana na moto na mafuriko ili kuepusha majanga zaidi,” alisema Bw Chege.

Mkurugenzi huyo  alisema kuwa kampuni hiyo imewekeza kwa makusudi katika kuboresha taasisi hiyo kwa lengo la kuimarisha uwezo wake wa kukabiliana na maafa na kuzima moto, mafunzo na kwingineko kwa ngazi ya juu.

Bw Chege alikuwa akizungumza katika taasisi hiyo tawi la Eldoret ambapo wafanyikazi kutoka sekta za umma na za kibinafsi walipata mafunzo ya siku mbili kukabiliana na majanga, mbinu za uokoaji na kuzima moto.

Alisema kuwa Taasisi ya Mafuta na Gesi ya Kenya Pipeline Company (KPC) Morendat  inatilia mkazo zaidi kujitayarisha kwa majanga, usalama mahali pa kazi na mbinu za kuzima moto ili kuhakikisha usalama unadumishwa.

“Ni jambo la busara kwa sekta ya umma na kibinafsi kuhakikisha kuna mipango faafu ya mafunzo kwa wafanyakazi ili kuwahami jinsi ya kukabiliana na majanga yanapotokea,” akasema Bw Chege.