Michezo

KPL kutoa uamuzi kuhusiana na gozi la Leopards, SoNy

April 16th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

MECHI ya mkondo wa pili ya Ligi Kuu kati ya SoNy Sugar na AFC Leopards inatarajiwa kuamuliwa leo Jumanne ama kama itarudiwa katika tarehe mpya au wenyeji SoNy wapoteze alama baada ya kutibuka Jumatatu ikiwa ni kwa siku ya pili uwanjani Awendo.

Mchuano huo wa raundi ya 23 ulikatizwa mnamo Aprili 14 jioni zikisalia dakika 25 utamatike baada ya mvua kubwa kuponda uwanja huo wa nyumbani wa SoNy.

Uliahirishwa hadi Aprili 15 kuanzia saa nne asubuhi, lakini haukuweza kuendelea baada ya mabingwa mara 13 Leopards kukataa kucheza kutokana na kukosekana kwa vifaa muhimu vinavyohitajika kama ambulensi.

Kisheria, lazima timu ilio nyumbani ahakikishie wageni usalama wao kwa kuwa na polisi wa kutosha pamoja na ambulensi ilio na vifaa vya matibabu.

Inasemekana mashabiki wa SoNy waliwazuia wachezaji wa Leopards kwa saa nzima kutoka uwanjani baada ya wageni kushikilia lazima vifaa hivyo viwepo kabla ya mechi kuendelea.

Nahodha wa SoNy, Enock Agwanda aliwatuliza mashabiki walioruhusu wachezaji wa Ingwe kuondoka uwanjani.

Afisa mmoja katika kampuni inayoendesha Ligi Kuu, KPL, alieleza Taifa Leo hapo Jumatatu kwamba “mechi yoyote haiwezi kuanza kabla ya ambulensi kuwasili kwa hivyo timu lazima zisubiri hadi ifike uwanjani.”

Aliongeza kwamba mechi hiyo itarudiwa, ingawa akasema hawezi kuzungumzia kama suala hili litashughulikiwa na Kamati Huru ya Nidhamu (IDCC).

Huku hayo yakijiri, hakuna mabadiliko kwenye jedwali la Ligi Kuu katika nafasi tatu za kwanza zinazoshikiliwa na Gor Mahia, Sofapaka na Bandari, mtawalia.

Hata hivyo, uongozi wa Gor wa alama tatu juu ya jedwali ulikatwa hadi tofauti ya magoli baada ya Sofapaka kulemea KCB 1-0 Jumapili.

Mashabiki wa klabu ya AFC Leopards washerehekea bao la Alex Orotomal, Ingwe ilipokabiliana na Thika United Agosti 18, 2018, uwanjani Thika. Picha/ Kanyiri Wahito

Gor na Sofapaka zimezoa alama 44 kila moja, ingawa mabingwa watetezi Gor wamesakata mechi nne chache.
Bandari ina alama 42 kutokana na mechi 22 baada ya kuchapa Western Stima 2-1.

Kakamega Homeboyz na Tusker zimeruka juu nafasi moja hadi nambari nne na tano zikiwa na alama 37 kila mmoja baada ya kushinda Vihiga United 1-0 na Kariobangi Sharks 2-0, mtawalia.

Mathare United imesukumwa chini nafasi mbili hadi nambari sita alama mbili nyuma.

SoNy inasalia ya saba kwa alama 34, tatu mbele ya Sharks.

Licha ya kupoteza mechi mbili mfululizo, KCB inasalia katika nafasi ya tisa kwa alama 29 sawa na Ulinzi Stars inayofunga 10-bora baada ya kuruka juu nafasi mbili.

Nzoia na Leopards zimezoa alama 28 na 27 mtawalia.

Zimeshuka chini nafasi moja kila mmoja. Stima na Chemelil Sugar zimesalia katika nafasi ya 13 na 14 kwa alama 26 na 25, mtawalia.

Posta Rangers imerukia nafasi ya 15 kwa alama 21 baada ya kupepeta wavuta-mkia Mount Kenya United 6-2. Vihiga ni ya 16 baada ya kuteremka nafasi moja.

Ina alama 20. Zoo na Mount Kenya zinashikilia nafasi mbili za mwisho kwa alama 17 na 12 mtawalia.