Michezo

KPL: Nick Mwendwa aendelea kulaumiwa kwa kutoa uamuzi wa 'mtu binafsi'

May 11th, 2020 1 min read

Na SAMMY WAWERU

HALI ya vuta n’kuvute inaendelea kushuhudiwa kuhusu mustakabali wa mechi za Ligi Kuu ya Kenya (KPL) 2020.

Licha ya Rais wa Shirikisho la Soka Kenya, FKF Nick Mwendwa kusimamisha kipute cha mwaka huu, baadhi ya wadau husika wanadai mechi lazima ziendelee.

Katika kauli ya hivi punde ya Afisa Mkuu Mtendaji wa FKF Barry Otieno, uamuzi wa kusimamisha michuano unapaswa kuafikiwa na wadau husika wote na wala si “mtu binafsi”.

“Michuano ya KPL haijaisha. Uamuzi wa Rais wa FKF ni batili na hauna maana yoyote,” amesema Bw Otieno mnamo Jumatatu.

Kulingana na afisa huyo, uamuzi wa kusimamisha michuano ya ligi unapaswa kushirikisha wadau husika wote, wafadhili, vilabu na viongozi.

Akisisitiza kipute kitaendelea, Otieno amesema hakuna mkutano uliofanyika kuafikia uamuzi wa Nick Mwendwa.

“Atuonyeshe kumbukumbu za mkutano,” akasema.

Janga la Covid-19 limeathiri shughuli nyingi nchini na ulimwengu kote michuano ya KPL 2020 na hafla za michezo zikisitishwa kuzuia maambukizi ya virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa huo.

Hata hivyo, wapo wanaohisi Rais wa FKF ametumia fursa hiyo kufuta michuano ya msimu huu ili kuanza upya mazungumzo na wafadhili na washirika kwa minajili ya msimu ujao.

Mkataba kati ya FKF na KPL unamalizika Septemba 2020 na FKF imeweka wazi haitatia upya saini mkataba huo ikieleza haja ya kujisimamia kuendeleza michuano ya ligi zijazo.

“Tunaheshimu sheria za serikali kuzuia maambukizi ya Covid-19. Sioni haja ya kusitisha michuano, ilhali kuna muda. Kufikia sasa hatujajua mshindi wa mwaka huu ni nani. Kabla ya Septemba 24, 2020, mkataba kati ya KPL na FKF kumalizika, ligi haipaswi kuathirika,” Otieno akaelezea.

Afisa Mkuu wa KPL Jack Oguda pia anasema uamuzi utatolewa baada ya mwezi Septemba na kwamba kauli za klabu husika zitachangia pakubwa.