Michezo

KPL sasa yasema ‘serikali saidia’ ikitangaza Ligi Kuu haiwezi kusimamishwa

October 18th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

Ligi Kuu ya soka ya Kenya (KPL) itaendelea jinsi ilivyopangwa, uongozi wa kampuni inayoendesha ligi hiyo KPL umesema na kuonya klabu lazima zifuate sheria zinazosimamia mchezo huo.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari Alhamisi, KPL ilisema ilifikia uamuzi huo, licha ya miito ya kutaka ligi isimamishwe kutokana na ukosefu wa fedha wa ligi na klabu baada ya mdhamini wake mkuu SportPesa kujiondoa.

“Hata hivyo, ligi hii imejitolea kuendelea kuimarisha bidhaa yake, kutumia soka kuleta mema, kuunga mkono ukuaji wa soka na kufanya shughuli hiyo kwa uadilifu ili kulinda sifa na uimara wake,” Afisa Mkuu Mtendaji wa KPL, Jack Oguda alisema.

Afisa huyo amefichua kuwa KPL imezungumza na kampuni kadha, lakini kutokana na hali mbaya ya kiuchumi, ofa zilizowekwa mezani hazifikii mahitaji ya Ligi Kuu.

“Inachukua muda kupata kandarasi rasmi kwa sababu kampuni nyingi zina bajeti zao, ambazo ziliwekwa mwanzo wa kipindi chao cha fedha,” alikariri Oguda.

Fedha

Aliitaka serikali iingilie kati kupeana suluhu ya muda mfupi ya kifedha ili ligi iendelee bila matatizo.

“Si siri kuwa klabu kadha zinatatizika kushiriki mechi humu nchini na za kimataifa, huku wachezaji na maafisa wakikodolea macho kupoteza kazi. Tunaomba pia Katibu katika Wizara ya Michezo, Utamaduni na Huduma za Jamii kuharakisha ujenzi wa uwanja wa kimataifa wa Nyayo, ambao ndio unafaa zaidi kutumiwa kwa ligi. Tunaomba pia serikali isaidie klabu kupigania mabadiliko ya sheria zinazosimamia michezo nchini na ambazo klabu zinaamini zitasaidia katika kuzifanya ziwe na uwezo wa kujikimu kifedha. Zaidi ya hayo, tunaomba serikali ipunguze ushuru kwa kampuni zinazosaidia michezo. Pia, tunaomba wadau (mashabiki, kampuni) kujitokeza kusaidia mchezo huu,” akasema.