Habari Mseto

KPLC yataka kila mteja aboreshe mita za tokeni lau sivyo stima itakatika

June 13th, 2024 1 min read

NA MUMBI WAINAINA

WATEJA wa kampuni ya Kenya Power and Lighting (KPLC) wanaotumia mita za kulipia kabla ya kutumia umeme wametakiwa kuziboresha kabla ya Agosti 31 au wakose huduma za stima.

Kampuni hiyo Jumatano ilizindua kampeni ya Update Token Meter Yako inayolenga wateja kubadilisha mita hizo kuwa za kisasa.

Mkurugenzi Mkuu wa KPLC, Dkt Joseph Siror alisema mita milioni 7.4 zinalengwa kwa shughuli hii.

Alisema shughuli hiyo haitaathiri bei ya tokeni.

“Habari njema ni kwamba hakuna mabadiliko ya bei, ni suala la tokeni mpya kuunganishwa na mfumo mpya ulioboreshwa na hakuna malipo,” Dkt Siror alisema.

KPLC inalenga kushughulikia changamoto nyingine ambazo hukabili wateja wanaolipia stima kabla ya kutumia, kufahamisha na kuelimisha umma kuhusu uboreshaji wa Mita ya Token.

Alisema ni shughuli ya kimataifa, katika nchi zote zinazotumia mita kulipia kabla kwa kutumia.

Dk Siror alisema asilimia 70 ya kukatika kwa umeme inasababishwa na miti.

“Itakuwa vyema ikiwa utaagizwa na wafanyakazi wa KPLC kuondoa miti iliyo karibu sana na laini zetu, ufanye hivyo,” Dkt Siror akasema.