Habari Mseto

KQ yaahirisha safari za Somalia hadi Desemba

November 15th, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Shirika la Ndege la Kenya Airways limetangaza kuahirisha uzinduzi wa safari zake za moja kwa moja kuelekea Mogadishu.

Sasa ziara hiyo itazinduliwa Desemba 5. KQ ilifaa kuzindua ziara hiyo ya moja kwa moja kutoka JKIA hadi Uwanja wa Kimataifa wa Aden Adde Alhamisi.

Hatua hiyo ilitarajiwa kuinua biashara kati ya mataifa hayo mawili. Katika taarifa Alhamisi, Mkurugenzi Mkuu wa KQ Sebastian Mikosz alisema ziara hiyo haitazinduliwa mpaka mahitaji ya utoaji huduma yatimizwe.

Kulingana naye, shirika hilo halikuwa na uwezo wa kuzuia utekelezaji wa hatua hiyo.

“Tunashirikiana na mamlaka husika kuhusiana na idhini muhimu na tunatarajia kumaliza utaratibu huo haraka iwezekanavyo ili tuanze rasmi operesheni,” alisema Bw Mikosz.

Ndege hiyo, Bombardier Dash 8 Q400, ya kila siku ya moja kwa moja itakuwa ikiondoka saa mbili kasoro dakika 20 asubuhi ili kufika Mogadishu 3.55 asubuhi.

Itakuwa ikiondoka Somalia saa 4.45 kufika Nairobi saa 7.00 mchana.