Habari

KQ yasema haisitishi safari za kuenda China, aghalabu kwa sasa

January 29th, 2020 1 min read

Na ALLAN OLINGO

SHIRIKA la ndege la Kenya Airways, KQ limesema Jumatano halisitishi kwa sasa safari za ndege hadi China licha ya kitisho cha virusi vya Corona, lakini likaeleza wazi kwamba linafuatilia hali halisi.

KQ inasema hivi huku shirika la ndege la Uingereza – British Airways – likitangaza kusitisha safari zake za kuingia Beijing na Shanghai baada ya serikali ya nchi hiyo kushauri raia wake wasisafiri kuenda China hasa ikiwa sababu si za lazima.

Kwa upande wa shirika la Kenya ni kwamba linafuatilia hali jinsi ilivyo na litachukua hatua madhubuti kwa wakati mwafaka.

“Kufuta safari za ndege ni mojawapo ya hatua tunazoweza kuchukua, lakini hili litatokea tu ikiwa tutabainisha kwamba ipo hatari ya wazi,” imesema KQ Jumatano.

Hii ni licha ya balozi wa Kenya nchini China Bi Sarah Serem kulishauri shirika hilo lisitishe safari zake za kuingia katika taifa hilo hadi virusi hivyo vidhibitiwe.

Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa KQ Allan Kilavuka amesema wanashauriana na serikali ya Kenya kuhusu ikiwa wanalazimika au ni lini watasitisha safari za ndege.

“Tunafuatilia matukio kila wakati na kila saa na tunashauriana na serikali kuhusu ni lini au ikiwa tunalazimika kusitisha safari,” amesema Bw Kilavuka.

Ndege za KQ huwa na safari tatu kila wiki za kutoka Nairobi-Guangzhou na Jumanne abiria wake mmoja aliwahiwa katika hospitali ya kitaifa ya Kenyatta (KNH) baada ya kushuka akitokea China akionyesha dalili za virusi hivyo ambavyo kufikia sasa vimewaua zaidi ya watu 130.

Kilavuka amesema ndege zinatunzwa likija suala la usafi na abiria wanavalia mavazi ya kuwakinga na kuzuia aina yoyote ya maambukizi ya Corona.

 

Kisa cha kwanza cha virusi hivyo kilitambulika Wuhan, katika mkoa wa Kati wa Hubei nchini China mnamo Desemba 2019.