Habari za Kitaifa

KRA yaagiza ushuru wa nyumba kutekelezwa kuanzia Machi 19

March 21st, 2024 1 min read

NA CHARLES WASONGA

MAMLAKA ya Kukusanya Ushuru Nchini (KRA) sasa imeagiza kuwa utozaji wa ushuru wa nyumba utekelezwe kuanzia Machi 19, 2024.

Kwenye taarifa Alhamisi, mamlaka hiyo imeagiza waajiri waanze kukata asimilia 1.5 ya mapato ya wafanyakazi wao kuanzia siku hiyo; siku moja baada ya Rais William Ruto kutia saini Mswada wa Nyumba za Gharama Nafuu 2023 kuwa sheria.

“Makato ya ushuru wa nyumba yalianza Machi 19, 2024. Kwa hivyo, waajiri wanahitajika kukata asilimia 1.5 kutoka kwa mishahara ya wafanyakazi wao na kuchangia kiasi sawa kama hicho kutoka kwa mshahara wa kila mwajiri,” KRA ikasema.

“Vile vile, watu wengine wanaochuma mapato nchini Kenya wanahitajika kuwasilisha asilimia 1.5 ya jumla ya mapato yao kama ushuru wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu (AHL) kwa KRA,” ikaongeza.

KRA ilifafanua kuwa tarehe ya kuwasilishwa kwa ushuru huo ni siku ya tisa ya mwezi ambapo mshahara huo ulistahili kulipwa au mapato hayo yalipokelewa

Mamlaka hiyo ilisema kuwa waajiri wanafaa kulipa pesa hizo kupitia benki zinazohudumu kama ajenti wa KRA au jukwaa la mtandao wa eCitizen kupitia nambari ya kufanya malipo (Pay Bill Number 222 222.

Kwa mujibu wa KRA, mchango wa waajiri katika ushuru wa nyumba ni makato yanayoruhusiwa chini ya Sehemu ya 15 ya Sheria za Ushuru wa Mapato.

Mamlaka hiyo imeonya kuwa mtu yeyote ambaye atafeli kulipa ushuru huo atapewa adhabu kwa kulipa asilimia tatu (3) ya pesa ambazo hazikulipwa kwa kila mwezi.

Mnamo Jumanne Rais Ruto alitia saini mswada wa Nyumba za Gharama Nafuu ya 2023 unaohalalisha ushuru huu.

Hii ni baada ya mswada huo kupitishwa katika katika Bunge la Kitaifa na Seneti baada ya kufanyiwa marekebisho.