Habari Mseto

KRA yanasa heroin iliyofichwa kwa ala za muziki JKIA

August 25th, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Mamlaka ya Kukusanya Ushuru (KRA) Jumatano ilikamata dawa za kulevya aina ya heroin za thamani ya Sh2.9 milioni katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta.

Maafisa wa KRA walisambaratisha mpango wa walanguzi wa kupitisha gramu 980 za dawa hizo ambazo walizipata katika uwanja wa DHL zikiwa zimefungwa kwa kifurushi.

Zilichunguzwa katika maabara ya KRA, forodhani, ambapo zilithibitishwa kuwa heroin.

Zilikuwa zimesafirishwa kutoka Mbarara, Uganda na zilikuwa zimefichwa kama vifaa vya usanii vya Kiafrika.

“Zilikuwa zikipelekwa katika Jimbo la Delta, Nigeria. Kifushi hicho kimepatiwa polisi wa kuchunguza na kudhibiti dawa za kulevya,” ilisema KRA katika taarifa.

KRA ilipata dawa hizo siku chache baada ya kupata dawa zingine zilizokuwa zimefichwa kama vitamin katika uwanja huo.