Habari Mseto

KRA yanasa Range Rover iliyofichwa kwenye kontena ikisingiziwa ni simiti

July 5th, 2019 1 min read

Na PETER MBURU

MAMLAKA ya Ukusanyaji Ushuru (KRA) imenasa lita 28,800 za ethanol ambayo hutumiwa kutengeneza pombe, pamoja na gari aina ya Range Rover Sports – linaloshukiwa kuibiwa Uingereza – katika Bandari ya Mombasa.

Mitungi 144 ikiwa na lita 200 za ethanol kila mmoja, ilipatikana katika kontena mbili za ukubwa wa futi mbili kwa 20, baada ya kontena hiyo kupitishiwa katika mashine za kukagua bidhaa bandarini.

Habari za kupotosha zilikuwa zimesema kuwa bidhaa zilizokuwa katika kontena hiyo zilikuwa ni magunia 1,000 ya simiti.

Katika kontena nyingine ya ukubwa wa futi 20, gari lilo la Range Rover Sports lilinaswa, japo nakala za bidhaa zilikuwa zimesema kuwa ndani mlikuwa na fremu za madirisha, milango, viti, stuli na picha za kutundika ukutani.

“Bidhaa hizo zilikamatwa kufuatia ripoti za kiujasusi; kontena zilipitishwa katika mashine za kukagua bidhaa za KRA ndipo picha zikaonyesha kuwa bidhaa zilizokuwa ndani hazikuwa zile nakala za usafiri wa bidhaa zilikuwa zikionyesha,” KRA ikasema katika taarifa kwa vyombo vya habari.

Timu iliyohusisha mashirika tofauti ya serikali na ambayo iliongozwa na KRA ilianzisha ukaguzi ndipo ikathibitisha kuwa kontena hizo tatu zilikuwa na lita 28,800 za ethanol iliyofichwa na gari hilo.