Habari za Kitaifa

KRA yataka malandilodi waongezee wapangaji kodi

May 9th, 2024 2 min read

NA DOMINIC OMONDI

MAMLAKA ya Ukusanyaji Ushuru Kenya (KRA) inaendelea kubuni mbinu mpya za kukusanya ushuru kwa kusukuma wamiliki wa nyumba za kukodisha kuongeza kodi wanayolipisha wapangaji.

Mamlaka hiyo haifurahii jinsi mapato ya wamiliki wa nyumba za kukodisha yanavyokosa kuongezeka kwa miaka mingi, hivyo basi hatua ya kuwasukuma itafanya kodi ya nyumba kupanda.

Kulingana na KRA, thamani ya nyumba inafaa kuwa ikiongezeka wala sio kukwama au kushuka kama mali nyingine za kuhamishika.

Ili kutimiza lengo lake, KRA imetumia wamiliki wa nyumba za kukodisha ilani baada ya kubaini kuwa ushuru kutoka kwa baadhi yao hauongezeki, kuashiria kuwa kodi haijaongezwa kwa muda au wanadanganya katika ulipaji wa ushuru.

Mamlaka hiyo imewataka wamiliki wa nyumba za kukodisha kuhakikisha kuwa kodi wanazotoza wapangaji zinawiana na thamani ya mali yao, kumaanisha wanawasukuma kuongeza kodi wanayotoza wapangaji.

Ingawa hatua hiyo inalenga kuwanasa malandilodi ambao wanadanganya wanapolipa ushuru wa nyumba zao, pia inaweza kuwaumiza wale ambao nyumba zao hazina wapangaji au kuwa na wapangaji wanaohama wanapoongezewa kodi.

Kupandishwa kwa kodi ya nyumba kutaumiza zaidi wafanyakazi ambao wanakabiliwa na mfumko wa gharama ya maisha ambao umekuwa ukiwahangaisha katika miaka ya hivi punde na kuwaacha bila pesa za matumizi.

“Kamishna (wa ushuru) amebaini kuwa mapato yako ya kodi kutokana na nyumba hayajabadilika au yamepungua kidogo kwa muda ambao umekuwa ukiyawasilisha,” KRA inasema katika ilani iliyotumia mmiliki mmoja wa nyumba mwezi Aprili ambayo Taifa Leo iliona.

“Tunaelewa kuwa kodi ya nyumba inapaswa kuwa ikiongezeka kulingana na uchumi na tunatarajia mawasilisho yako ya mwezi huu yataakisi hayo na iwapo uliyowasilisha awali yanaweza kubadilishwa, kuwasilisha sifuri au kukataa kuwasilisha mapato ya kodi ya nyumba hakuruhusiwi kamwe,” KRA inaongeza.

Hatua hii inaweza kusababisha mzozo mpya kati ya KRA na wamiliki wa nyumba ambao wanasema hali ngumu ya uchumi imewafanya kutoongeza kodi ili wapangaji wasihame.

Kuanzia Januari, wamiliki wa nyumba wanatakiwa kulipa Ushuru wa Mapato ya Kodi ya Nyumba kila mwezi wa asilimia 7.5 ya jumla ya pesa zote wanazokusanya kutoka kwa wapangaji.

Awali, walikuwa wakilipa asilimia 10 ya kodi baada ya kutoa gharama zao ikiwemo mikopo na urekebishaji.

Ushuru huu unapaswa kulipwa na watu wote wanaoingiza mapato ya kodi ya nyumba ya kati ya Sh280,000 na Sh15 milioni. Sasa, wanapaswa kulipa ushuru huo kwa pesa wanazopata kabla ya kutoa gharama yoyote.

Mmoja wa wamiliki wa nyumba wanaolengwa ana majumba matatu Mlolongo, Kaunti ya Machackos.

Anasema kwa miaka kadhaa amekuwa akilipa ushuru wa mapato ya kodi kila mwezi kwa KRA.

“Mapato ya kodi ya nyumba huwa yanaongezeka kila ninapopata mpangaji mpya lakini sio kwa kuwa wameishi kwa miaka mingi. Kupata mpangaji wa kudumu sio rahisi na kwa hivyo siwaongezei renti,” alisema kwa sharti asitajwe jina kwa kuhofia kuchukuliwa hatua na KRA.

“Kuna nyumba nyingi za kukodisha katika mtaa ambao zangu zipo na iwapo utapandisha renti, wapangaji watahamia nyumba nyingine,” alisema.

Agizo hilo la KRA ni miongoni mwa mengine ambayo yamemlimbikizia Mkenya kodi chini ya utawala wa Rais William Ruto.

Baadhi ya kodi au nyongeza za kodi zilizosukumiwa Wakenya ni ushuru wa mafuta (VAT) kutoka asilimia nane hadi 16, Ushuru wa Nyumba asilimia 1.5, Ushuru wa Mapato ya Biashara ndogondogo kutoka asilimia 1.5 hadi 3 ya jumla ya mapato wala si faida, na ushuru wa bidhaa za kuagiza kutoka nje ya nchi wa asilimia 2.5 kutoka 1.5.

Ushuru huo mpya au nyongeza ya kodi ulibuniwa na Sheria ya Fedha ya 2023.

Mahakama iliharamisha Ushuru wa Nyumba ambao pia hutozwa waajiri kwa asilimia 1.5 kwa kuwa ulikuwa wa kibaguzi. Hata hivyo serikali ilirekebisha vipengee vilivyouharamisha ushuru huo kabla ya kuanza kukata wafanyakazi tena.