Habari Mseto

KRA yazuilia watu 21 wa kigeni waliotwaa magari kutoka kwa Wakenya

May 24th, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

MAMLAKA ya Kukusanya Ushuru nchini (KRA) imekamata magari 21 yaliyo na nambari za usajili za mataifa mengine ya thamani ya Sh30 milioni.

Magari hayo yalikamatwa Jumamosi Mei 19, wakati wa operesheni maeneo ya Mombasa, Lunga Lunga na Taveta.

Magari hayo yalizuiliwa baada ya wamiliki wake kushindwa kutoa vyeti rasmi vya kumiliki magari hayo.

Maafisa wa KRA walikuwa katika operesheni ya kumaliza bidhaa ghushi, zilizopigwa marufuku nchini na magari yaliyoagizwa nchini kinyume cha sheria.

Magari hayo yalitwaliwa kutoka kwa Wakenya, kinyume cha sheria, licha ya kuwa na nambari za usajili za mataifa ya kigeni.

Kulingana na taarifa ya KRA, watakaopatikana na makosa wataadhibiwa kuambatana na sheria, au watalazimnishwa kufuata sheria kuyapata magari hayo nchini.

Magari yaliyoagizwa na yatakayopatikana kuwa zaidi ya miaka minane yataharibiwa, ilisema KRA katika taarifa.