Habari Mseto

KRISMASI: Afariki baada ya kubugia pombe kupindukia

December 27th, 2018 1 min read

Na WAANDISHI WETU

MWAMAMUME alifariki baada ya kunywa pombe kupita kiasi wakati wa sikukuu ya Krismasi huku wenzake wakiokolewa na wahudumu wa afya.

Kisa hicho kilitokea katika kijiji cha Rambugu, eneobunge la Rarieda, Kaunti ya Siaya

Mwuguzi msimamizi wa zahanati ya Rambugu, Bi Lucy Owiyo, alithibitisha kuwa Bw Onyango Yongo, 55, alifikishwa hospitalini akiwa amefariki baada ya kutapika na kuzimia kufuatia unywaji pombe siku nzima kwenye karamu ya Krismasi.

Wenzake wawili ambao pia walikuwa wamezimia walitibiwa na kuruhusiwa kwenda nyumbani.

Katika kisa kingine kuhusiana na sherehe za Krismasi, mtoto mwenye umri wa miaka mitano alichomeka hadi kufa nyumbani kwao alikoachwa siku ya Krismasi usiku na mamake aliyedaiwa kwenda kilabuni kujiburudisha.

Kulingana na majirani katika mtaa wa mabanda wa Obunga katika Kaunti ya Kisumu, waliona moshi na moto kutoka nyumbani humo lakini baada ya kujikakamua na kuuzima wakapata mwili wa mtoto huyo.

Kamanda wa Polisi Kaunti ya Kisumu, Job Boronjo alithibitisha kisa hicho na kuongeza kuwa walikuwa wakimtafuta mama huyo.

Alisema atafunguliwa mashtaka ya kumtelekeza mwanawe huku uchunguzi ukiendelezwa kubainisha chanzo halisi cha kifo cha mtoto huyo

“Kulingana na uchunguzi wetu, mama huyo alikuwa ameenda kwenye kilabu kilicho karibu na kuacha amemfungia mtoto huyo ndani ya nyumba. Wakati majirani walimfahamisha kuhusiana na kisa hicho tayari alikuwa mlevi,” alisema Boronjo.

“Usalama wa mtoto ni muhimu kuliko burudani. Polisi watamfungulia mashtaka,” alisema kamanda huyo.

Katika Kaunti ya Kilifi, Kamanda wa Polisi Bw Frederick Ochieng’, alithibitisha kisa ambapo wanafunzi wawili wa Chuo Kikuu cha Pwani walifariki wakiogelea, mmoja baharini na mwingine hotelini.

Alisema katika siku za usoni wasimamizi wa hoteli watakuwa wakishtakiwa kwa uzembe ikiwa watu watafariki kwenye vidimbwi wanavyosimamia.

Katika eneo la Awendo, Kaunti ya Migori, polisi wanamtafuta mwanamume aliyesemekana kuvunja nyumba ya jirani yake na kumbaka.

Ripoti za Elizabeth Ojina, Vivere Nandiemo, Rushdie Oudia na Charles Lwanga