Habari

KRISMASI: Bei ya nyama ya mbuzi na kuku yapanda

December 24th, 2019 1 min read

JOHN MUTUA na CHARLES WASONGA

BEI ya mbuzi na kuku imepanda zaidi wakati huu wa Krismasi huku uchumi ukishuhudia kupungua kwa watu wanaonunua kuwageuza kitoweo.

Mbuzi mzima katika soko maarufu ya nyama ya mbuzi ya Kiamaiko, katika mtaa wa Huruma, Nairobi inauzwa kwa Sh8,000 kutoka bei ya kawaida ya Sh4,000 huku wafanyabiashara wakiimarisha mauzo yao wakati huu wa msimu wa sherehe.

Bei ya kuku katika soko la Burma, Nairobi imepanda na kufikia kati ya Sh1,300 na Sh1,500 kutoka bei ya kawaida ya wastani ya Sh1,000.

Kupanda huku kwa bei kunajiri wakati ambapo uchumi nchini umezorota.

“Bei zimepanda lakini wananchi wanakabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi na wateja ni wachache. Hapo awali ningeweza kuwauza kuku 30 kwa siku, lakini sasa idadi hiyo imepungua hadi kuku 10 pekee kwa siku. Hali sio nzuri,” akasema Faith Munyiva, ambaye amekuwa akiendesha biashara ya kuuza kuku katika soko hilo la Burma tangu mwaka wa 2000.

Wiki hii mfanyabishara huyu alikuwa na kuku 300 lakini kufikia Jumanne hakuwa ameuza wote.

Naye Protus Onyango ambaye ni muuza nyama katika soko hilo hilo la Burma pia anasema biashara sio nzuri ikilinganishwa na miaka ya nyuma. Mfanyabiashara huyo hununua nyamba ya mbuzi kutoka soko la Kiamaiko ambako kuna kichinjio kikubwa.

“Wateja ni wachache kwa sababu watu wengi wamesafiri kwenda mashambani na familia zao. Tutapata wateja wapi?” akashangaa.

Bw Onyango anaongeza kuwa bei ya wastani ya kilo moja ya nyama haipiti Sh400, lakini sasa wanalazimika kuuza nyama kwa Sh300.

Nyama ya mbuzi na kuku hupendwa zaidi na Wakenya wakati kama huu wa msimu wa sherehe.