Habari

Krismasi: Huduma za paspoti zasitishwa hadi Ijumaa

December 24th, 2019 1 min read

Na CHARLES WASONGA

IDARA ya Uhamiaji imesitisha shughuli za utoaji paspoti hadi Ijumaa wiki hii.

Kulingana na ujumbe ambao idara hiyo iliweka Jumanne katika akaunti yake ya twitter, hatua hiyo imechukuliwa “ili kutoa nafasi kwa ukarabati wa dharura wa mitambo”.

“Huduma za utoaji paspoti zimesitishwa Jumanne kutokana na ukarabati ambao haukuratibiwa hapo awali. Shughuli za kawaida zinarejea Ijumaa Desemba 27, 2019,” idara hiyo ilisema, ikiongeza kuwa hali hatua hiyo imechukuliwa kutoka na “sababu ambazo hazingeepukika.”

Hii ina maana kuwa maelfu ya watu ambao Jumanne walijitokeza kusaka huduma za paspoti katika vituo mbalimbali walilazimika kurejea nyumbani baada ya kukosa huduma hizo.

Foleni ndefu zimekuwa zikishuhudiwa katika afisi za idara ya uhamiaji kote nchini kuwasilisha maombi ya kupewa paspoti mpya ya kieletroniki, kuelekea kuzimwa kwa paspoti za kisasa za muundo wa zamani.

Inakadiriwa kuwa angalau Wakenya milioni moja wametuma maombi ya paspoti hiyo mpya huku takriban Wakenya 1.5 milioni wakiendelea kutumia paspoti za zamani, kulingana na takwimu zilizotolewa na Idara ya Uhamiaji.