Dondoo

KRISMASI: Polo aliyedai ameenda kesha atiwa adabu na kisura alipofumaniwa kwa mama pima

December 27th, 2018 1 min read

Na TOBBIE WEKESA

Adanya, TESO

Kizaazaa kilizuka katika boma moja la hapa baada ya kipusa kumpa mumewe kichapo kikali alipompata kwa mama pima ilhali alidai alikuwa kesha kanisani.

Inasemekana kipusa aliudhika sana alipomkuta polo kwa mama pima akisata densi ilhali alitoka nyumbani akidai alikuwa akienda kesha kanisani. Inadaiwa baada ya kupata mlo wa jioni, polo alimueleza mke wake kwamba alitaka kwenda kanisani kwa ibada ya kusherehekea kuzaliwa kwa Yesu Kristo.

“Mwaka huu wote nadhani ulienda kanisani mara chache sana. Inakuaje leo unaenda kesha na vile kuna baridi hivi?” kipusa alimuuliza polo. ?Kulingana na mdokezi, polo alimueleza kipusa kwamba alitaka kubadilisha maisha.

Baada ya jamaa kuondoka mkewe alimfuata na kupata wanaume wachache mno sana kanisani na mumewe hakuwepo. Kipusa aliamua kuelekea kwa boma moja kulikokuwa kunatokea muziki.

Duru zinasema kipusa alipigwa na butwaa kumpata mumewe akisakata densi akiwa na warembo.

“Hili ndilo kanisa ulilokuwa ukiniambia unaenda! Nikupate nyumbani haraka!” mwanadada alimkaripia polo. Polo alichomoka polepole na kuelekea alikokuwa mkewe.

“Unafikiri mimi ni mjinga. Unaniacha kwa baridi huku ukiniambia unaenda kusali kumbe unakuja kubanjuka hapa na mama wazee,” kipusa alimshtumu polo huku akimpa makofi. Duru zinasema polo alimuomba kipusa msamaha lakini wapi.

“Wewe umezoea kunidanganya. Leo lazima upate adabu,” kipusa alimkemea polo huku akiendelea kumpa kichapo. Inasemekana ilibidi polo achomoke mbio hadi nyumbani baada ya kuona kipusa hakuwa tayari kumsamehe.

Waliokuwemo walishangaa kuona jamaa alivyokuwa amekaliwa chapati na mkewe. Hata hivyo baadhi walisema jamaa alikosea kwa kudanganya mkewe alikuwa akienda kanisa na kwenda kuponda raha na wanawake kwa mama pima.