Habari Mseto

Krismasi: Wafungwa wafurahia mapochopocho na vinywaji

December 24th, 2018 1 min read

Na MAGDALENE WANJA

Wafungwa katika gereza la Nakuru GK walipata nafasi ya kusherehekea Krismasi ya mapema hapo Jumapili baada ya wasamaria wema kuwaletea mapochopocho, vinywaji na zawadi ainati.

Wafungwa hao walifurahia vyakula mbalimbali kama vile wali, chapati na nyama vilivyoandaliwa na shirika la muungano wa dini mbalimbali lijulikanalo kama World Kingdom Service Ministry.

Tabasamu yahitajika wakati wasamaria wema wamejitolea kuandaa mlo wa aina yake. Picha/ Maggy Wanja

Kulingana na waandalizi wa hafla hiyo, chaguo la kusherehekea pamoja na wafungwa hao ilikuwa ni kuwapa nafasi ya kufurahia licha ya kuwa mbali na jamaa zao.

“Sio chakula tu bali pia kuwaonyesha upendo na kuwahubiria neon la mUngu na kuwapa tumaina ata wanapoendelea kutumikia vifungo mbalimbali,” alisema Bi Alice Mugure ambaye ni mwanzilishi wa shirika hilo.

Raha tupu huku wakila chakula walichokikosa kwa muda mrefu. Picha/ Maggy Wanja

Wafungwa hao vilevile waliandaa michezo mbalimbali ikiwemo kandanda kama njia ya kutangamana.

“Tumefurahia sana kwa mlo ambao ni wa kipekee amabo hatupati siku za kawaida na vilevile kupata wageni ambapo sio jambo la kawaida,” alisema Bw Samuel Kipkemoi.

“Sio jambo la kawaida kwa jambo kama hili kufanyika na inatokana na upendo na kujitolea,” aliongeza Bw Willis Nandi ambaye amekuwa kwa jela hiyo kwa miaka 19.

Waliungana kuitafuna minofu ya nyama waliyoandaliwa. Picha/ Maggy Wanja

Afisa msimamizi wa gereza hilo Bw Japheth Onchiri alisema kuwa hafla kama hii huwapea nafasi wafungwa kuhisi kama binadamu wengine ata wanapotumikia vifungo mbalimbali.

Bw Onchiri aliwapa changamoto wananchi kuonyesha ukarimu wao wakati wa hafla za Krisimasi kwa kuwakumbuka wasiojiweza kama vile wafungwa.