Habari Mseto

KRISMASI: Watoto 30 wazaliwa Desemba 25

December 27th, 2018 1 min read

Na WAANDISHI WETU

WATOTO zaidi ya 30 walizaliwa wakati wa Krismasi katika hospitali kadha kuu nchini wakiwemo pacha wa wavulana waliozaliwa Hospitali ya Kenyatta Desemba 25.

Jumla ya watoto ishirini walizaliwa katika hospitali hiyo siku ya Krismasi.

Kulingana na hospitali hiyo, watoto kumi walikuwa wasichana nao kumi wakiwa wavulana.

Tabasamu zilijaa kwenye nyuso za akina mama hao licha ya uchungu wa uzazi wa uliopita na kusema kuwa sasa watakuwa wakisherehekea Krismasi kwa furaha zaidi baada ya kujifungua siku hiyo ya kipekee ulimwenguni.

Katika hospitali kuu ya rufaa ya Kaunti ya Embu, watoto wanane walikaribishwa duniani kwa shangwe.

Kwa mujibu wa mwuguzi mkuu aliyekuwa kwenye zamu katika hospitali hiyo ya Embu Referral Level Five, watoto 11 walikuwa wasichana huku watatu wakiwa wavulana.

Watoto wote walikuwa na uzito wa kati ya kilo 2.5-4 na wako katika hali shwari licha ya watano kuzaliwa kupitia upasuaji, alisema afisa mkuu wa uuguzi Bi Mary Njue.

Vilevile, mama zao wataruhusiwa kwenda nyumbani hivi karibuni.

“Watoto wako sawa kiafya na mama zao wanasherehekea. Sisi kama wakunga pia tuko na furaha kwa sababu hakuna mama hata mmoja alipatwa na matatizo,” Bi Njue aliambia Taifa Leo katika ofisi yake hospitalini humo.

Alisema akina mama hao walilazwa katika hospitali ya Embu Referral Level Five wakiwa na uchungu mkali wa uzazi, na kufululizwa mara moja hadi chumba cha kujifungua.

Bi Njue alieleza: “Tuliwashughulikia haraka na kwa bahati nzuri walijifungua watoto wenye afya tele. Na sasa kwa sababu wako katika hali nzuri wataruhusiwa kwenda nyumbani hivi karibuni ili waungane na jamaa zao kuendelea sherehekea sikukuu.”