Habari Mseto

KRISMASI: Watu 10 wakosa kuona siku muhimu

December 24th, 2019 2 min read

Na WAANDISHI WETU

SHEREHE za Krisimasi ziligeuka kuwa huzuni kwa familia kadhaa huku watu 10 wakifariki kwenye ajali katika sehemu mbalimbali nchini jana.

Katika Kaunti ya Busia, familia mbili zinaomboleza baada ya jamaa zao watano kufariki kwenye ajali mbaya iliyofanyika jana asubuhi katika barabara ya Mumias-Butere katika Kaunti ya Kakamega.

Watano hao walikuwa wakielekea jijini Nairobi kwa sherehe za Krisimasi.

Wanajumuisha mwanamume, mkewe, msichana wao wa miaka 10 na mwanafunzi aliyehitimu majuzi kutoka chuo kikuu. Mwanafunzi huyo anatoka katika familia tofauti. Hata hivyo, wote wanatoka katika kijiji kimoja katika eneo la Butula, Kaunti ya Busia. Walikuwa sehemu ya kundi la watu waliokuwa wakisafiria gari moja.

Gari lao aina ya Toyota Wish lenye nambari ya usajili KCD 286B lilianguka katika Mto Lilondwe baada ya kupoteza mwelekeo.

Kulingana na Kamanda wa Polisi katika Kaunti Ndogo ya Mumias, Bw Peter Kattam, gari hilo lilikuwa na abiria 10.

Katika Kaunti ya Kirinyaga, wanafunzi wawili walifariki baada ya kuhusika kwenye ajali mbaya ya barabarani.

Wawili hao walifariki baada ya pikipiki waliyokuwa wakisafiria kuligonga gari aina Toyota Land Cruiser kutoka nyuma katika barabara ya Gakoigo-Njegas. Ajali hiyo ilifanyika katika kijiji cha Kiamuthambi, hali iliyowaacha wenyeji kwa mshangao.

Mmoja wa wale waliofariki ni mwanafunzi wa kidato cha tatu huku mwenzake akiwa mtahiniwa wa kidato cha nne aliyekamilisha masomo yake juzi. Alitarajiwa kujiunga na chuo kikuu.

Walioshuhudia walisema kwamba pikipiki hiyo ilipoteza mwelekeo na kugonga gari hilo lililokuwa likielekea mjini Kerugoya.

“Wanafunzi walikuwa wakiendesha pikipiki hiyo. Walipata majeraha mabaya ya kichwa. Ilikuwa vigumu kwao kunusurika,” akasema Bw Jeremiah Mwangi, mmoja wa walioshuhudia ajali hiyo.

Bw Mwangi alisema kuwa ni tukio la kuhuzunisha kwa wanafunzi hao kufariki kupitia ajali. Mtu mwingine alisema kwamba alikuwa nyumbani kwake aliposikia sauti kubwa na alipokaribia mahali pa tukio akakuta waathiriwa wameloa damu.

Katika Kauti ya Bomet, mtu mmoja alifariki jana huku wengine wawili wakijeruhiwa katika ajali iliyofanyika katika kituo cha kibiashara cha Kapkwen, kwenye barabara ya Kaplong-Bomet.

Katika Kaunti ya Nakuru, watu wawili walifariki Jumatatu usiku baada ya gari walimokuwa wakisafiria kugongana ana kwa ana na ambulensi kwenye barabara ya Nakuru-Subukia.

Kamanda wa Polisi katika Kaunti Ndogo ya Subukia, Bw Edward Imbwaga alithibitishia kuwa ambulensi hiyo ilikuwa ya Hospitali ya Subukia.

Kulingana naye, matatu iliyohusika kwenye ajali ni ya shirika la 4NTE Sacco ilikuwa ikielekea Nakuru kutoka Subukia.

Aliongeza kuwa ambulensi hiyo ilikuwa na watu wawili lakini haikubainika ikiwa mtu wa pili alikuwa mgonjwa.

“Waliojeruhiwa ni dereva wa ambulensi na abiria wengine 12 ambao walikuwa ndani ya matatu hiyo,” akasema.

Shaban Makokha, George Munene, Phyllis Musasia na Vitalis Kimutai