Habari Mseto

Krismasi ya ajali

December 24th, 2018 2 min read

PIUS MAUNDU na JOHN NJOROGE

WATU kumi wakiwemo maafisa watatu wa KDF waliaga dunia katika ajali mbili tofauti kwenye barabara kuu ya Mombasa-Nairobi Jumapili. 

Ajali ya kwanza ilitokea eneo la Kanga karibu na mji wa Mtito Andei na kuangamiza watu sita papo hapo, wakati magari mawili ya kibinafsi yaligongana ana kwa ana.

“Gari lililokuwa likielekea Mombasa lilikuwa likipita lori wakati ajali hiyo ilitokea,” kamishna wa kaunti ya Makueni Mohammed Maalim akasema.

Alisema kuwa walioumia walipelekwa katika hospitali ya Voi, huku magari hayo yakivutwa hadi kituo cha polisi cha Mtito Andei.

Eneo la Mlima Kiu karibu na soko la Salama, takriban kilomita 250 kutoka hapo, lori la KDF lilibingirika baada ya dereva kupoteza mwelekeo alipokuwa akiteremka.

“Afisa mmoja alikufa papo hapo nao wawili wakaaga dunia walipokuwa wakikimbizwa hospitalini. Maafisa saba walipata majeraha mabaya na wakafikishwa katika hospitali ya rufaa ya Machakos naye mmoja akikosa kujeruhiwa,” OCPD wa Mukaa Charles Muthui akaeleza Taifa Leo.

“Lori hilo lilikuwa likisafiri kutoka Kahawa Barracks kuelekea Mombasa wakati ajali hiyo ilipotokea,” afisa mmoja wa KDF ambaye alifika eneo la ajali kuokoa wenzake akasema.

Mili ya wanajeshi hao ilipelekwa katika hifadhi ya maiti ya hospitali hiyo ya rufaa ya Machakos, nalo lori likavutwa hadi kituo cha polisi cha Salama.

Ajali hizo zilitokea saa chache baada ya nyingine iliyohusisha pikipiki eneo la Wote na kusababisha kifo kwa afisa wa gereza la Makueni.

“Mmoja wa waendeshaji wa pikipiki hizo alikuwa akijaribu kuvuka gari ndipo wakagongana ana kwa ana. Afisa huyo ambaye alikuwa akiendesha pikipiki aliumia kichwani na kufariki muda mfupi baada ya mkufikishwa hospitalini,” OCPD wa Makueni Bosita Omukolongolo akasema, kuhusu ajali hiyo ya jana.

Kwingineko, mtu mmoja alifariki huku wengine saba wakipata majeraha mabaya kwenye ajali ya barabarani iliyofanyika Jumamosi usiku katika eneo la Salgaa katika barabara ya Nakuru-Eldoret.

Ajali hiyo ilihusisha magari manne yakiwemo lori, magari mawili ya kibinafsi na matatu. Magari hayo yote yalikuwa yakielekea mjini Nakuru kutoka Eldoret.

Kulingana na walioshuhudia, aliyefariki ni dereva wa trela hilo ambalo lilikuwa limeegeshwa kando ya barabara.

Walioshuhudia walisema kwamba ajali hiyo ilifanyika baada ya dereva kupoteza udhibiti wa trela hilo.

“Trela hilo lilikuwa likienda kwa mwendo wa kasi kabla ya kupoteza mwendo na kugonga mojawapo ya magari hayo. Baadaye, lililigonga trela ambalo lilikuwa limeegeshwa. Kuna uwezekano trela lilipata hitilafu za kimitambo,” akasema Bi Rachel Maru, ambaye alishuhudia ajali hiyo.

Wakati wa ajali hiyo, mtu mmoja alivunjika miguu yake.