KRU kuwa mpatanishi wa amani kati ya Pokot na Marakwet, polisi na bodaboda Kajiado

KRU kuwa mpatanishi wa amani kati ya Pokot na Marakwet, polisi na bodaboda Kajiado

Na GEOFFREY ANENE

SHIRIKISHO la Raga Kenya (KRU) linapanga kufanikisha mazungumzo ya amani kati ya jamii za Pokot na Marakwet katika mojawapo ya njia inapanga za kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Michezo kwa Maendeleo na Amani (IDSDP) hapo Aprili 28.

Pia, litaongoza mazungumzo ya amani kati ya maafisa wa polisi na bodaboda wa mji wa Kajiado. Mazungumzo mengine ya amani yatakayoongozwa na KRU ni kati ya jamii za Samburu na Borona mjini Isiolo.

“Mashirikisho yanayosimamia raga nchini Kenya (KRU) na barani Afrika (Rugby Africa) yameandaa shughuli nne kusherehekea siku hiyo kote nchini. Mojawapo ya malengo familia ya raga inalenga kutimiza ni kuwapa tumaini kupitia mifano ya kimichezo,” KRU ilisema.

Mazungumzo ya amani kati ya Pokot na Marakwet yataongozwa na afisa wa maendeleo ya eneo la Bonde la Ufa, Basemath Nyabando.

Sarah Atieno na David Weru wametwikwa majukumu ya mazungumzo ya amani kati ya polisi wa Kajiado na bodaboda mjini humo naye Patrick Mwika anayesimamia maendeleo ya eneo la Mlima Kenya atakuwa mjini Isiolo kwa mzungumzo ya amani kati ya jamii za Samburu na Borana.

Shughuli ya nne, KRU inasema, itakuwa warsha ya kupitia mtandao itakayoandaliwa na Afisa wa Maendeleo wa KRU Ronnald Okoth pamoja na Kituo cha Kimataifa cha Mafunzo ya Kusaidia katika masuala ya amani kinachoendeshwa na Jeshi la KDF (IPSTC).

“Mada ya warsha hiyo ni “kufanikisha amani pamoja” na tutakuwa na wasemaji sita wa kuhamasisha. Wazungumzaji ni wachezaji wawili kutoka timu ya taifa ya raga ya wachezaji saba kila upande maarufu kama Shujaa na mwingine ni afisa wa kurekebisha tabia katika Idara ya Magereza. Watazungumzia jinsi maisha yao yamebadilishwa na maadili ya raga: uadilifu, uchu, nidhamu, mshikamano na ushirikiano.

Wazungumzaji wengine ni Kapteni Idris Miriam na Luteni Kanali Mwasaru wanaosimamia IPSTC pamoja na wahadhiri wawili kutoka kituo hicho Dkt Michael Sitawa na Michael Osew Ngachra.

  • Tags

You can share this post!

Bayern Munich wakomoa Leverkusen 2-0 na kunusia taji la...

Makocha wa voliboli kutoka Brazil sasa wachukua usukani wa...